Chapter 15
1 Sasa ndugu, napenda kuwakumbusha ile Habari Njema
niliyowahubirieni nanyi mkaipokea na kusimama imara ndani yake.
2 Kwa njia yake mnaokolewa, ikiwa mnayazingatia maneno
niliyowahubirieni, na kama kuamini kwenu hakukuwa bure.
3 Mimi niliwakabidhi ninyi mambo muhimu sana ambayo mimi
niliyapokea: kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na
Maandiko Matakatifu;
4 kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kama
ilivyoandikwa;
5 kwamba alimtokea Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na
wawili.
6 Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano kwa mara moja;
wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa.
7 Baadaye alimtokea Yakobo kisha akawatokea mitume wote.
8 Baada ya wote, akanitokea hata mimi, mimi niliyekuwa kama
mtu aliyezaliwa kabla ya wakati.
9 Maana mimi ni mdogo kabisa miongoni mwa mitume na wala
sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililidhulumu kanisa la Mungu.
10 Lakini, kwa neema yake Mungu, nimekuwa kama nilivyo. Na
neema yake kwangu haikuwa bure. Mimi nimefanya kazi kuliko wote; si mimi hasa,
ila ni neema ya Mungu ifanyayo kazi pamoja nami.
11 Lakini hata hivyo, iwe wao ndio wahubirio au mimi
nihubiriye, haidhuru, hiki ndicho tunachuhubiri, na hiki ndicho mnachoamini.
12 Sasa, maadam inahubiriwa kwamba Kristo amefufuliwa
kutoka wafu, baadhi yenu wanawezaje kusema kwamba hakuna ufufuo wa wafu?
13 Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye
hakufufuka;
14 na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana
maana na imani yenu haina maana.
15 Zaidi ya hayo sisi tungekuwa mashahidi wa uongo mbele ya
Mungu, maana tulisema kwamba Mungu alimfufua Kristo kutoka wafu na kumbe yeye
hakumfufua - kama ni kweli kwamba wafu hawafufuliwi.
16 Maana, ikiwa ni kweli kwamba wafu hawafufuki, basi naye
Kristo hakufufuka.
17 Na kama Kristo hakufufuliwa, basi, imani yenu ni ya
bure; mngali bado katika dhambi zenu.
18 Zaidi ya hayo, wale wote waliokufa wakiwa wameungana na
Kristo wamepotea kabisa.
19 Kama matumaini yetu katika Kristo yanahusu tu maisha
haya ya sasa, basi, sisi ni watu wa kusikitikiwa zaidi kuliko wengine wote
duniani.
20 Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka wafu,
limbuko lao wale waliolala katika kifo.
21 Maana kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja,
vivyo hivyo nako kufufuka kutoka wafu kumesababishwa na mtu mmoja.
22 Kama vile watu wote wanavyokufa kwa kujiunga na Adamu,
vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo.
23 Lakini kila mmoja kwa mpango wake: Kristo kwanza, halafu
wale walio wake Kristo wakati Kristo atakapokuja.
24 Baada ya hayo, mwisho utafika wakati ambapo Kristo
atamkabidhi Mungu Baba Utawala, baada ya kufutilia mbali kila tawala na mamlaka
na nguvu.
25 Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda
adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake.
26 Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni kifo.
27 Maana, Maandiko yasema: "Mungu ameweka vitu vyote
chini ya miguu yake." Lakini, Maandiko yanaposema: "Vitu vyote
vimewekwa chini ya miguu yake avitawale" ni dhahiri kwamba Mungu haingii
katika kundi hilo la vitu, maana yeye ndiye anayeviweka vitu hivyo chini ya
Kristo.
28 Lakini vitu vyote vitakapowekwa chini ya Utawala wa
Kristo, ndipo naye Mwana atakapojiweka chini ya Mungu, aliyeweka vyote chini ya
Utawala wake; ili Mungu atawale juu ya vyote.
29 Kama hakuna ufufuo, je watu wale wanaobatizwa kwa ajili
ya wafu wanatumainia kupata nini? Kama wafu hawafufuliwi, ya nini kubatizwa kwa
ajili yao?
30 Na sisi, ya nini kujitia hatarini kila saa?
31 Ndugu, mimi nakikabili kifo kila siku! Fahari niliyo
nayo juu yenu katika kuungana na Kristo Yesu Bwana wetu inanifanya nitangaze
jambo hili.
32 Kama kusudi langu lingalikuwa la kibinadamu tu, kule
kupigana kwangu na wanyama wakali hapa Efeso kungalinifaa kitu gani? Kama wafu
hawafufuki, basi, "Tule na tunywe, maana kesho tutakufa."
33 Msidanganyike! Urafiki mbaya huharibu tabia njema.
34 Amkeni! Anzeni kuishi vema, na acheni kutenda dhambi.
Baadhi yenu hawamjui Mungu kabisa. Hii nawaambieni, ni aibu kubwa kwenu!
35 Lakini mtu anaweza kuuliza: "Wafu watafufuliwaje?
Watakuwa na mwili wa namna gani wakati watakapokuja tena?"
36 Hayo ni maswali ya kijinga! Ukipanda mbegu, isipokufa
kwanza haitaota.
37 Unachopanda ni mbegu tu, labda ya ngano au nafaka
nyingine, na si mmea mzima ambao hutokea baadaye.
38 Mungu huipa hiyo mbegu mwili anaoutaka mwenyewe; kila
mbegu hupata mwili wake wa pekee.
39 Miili ya viumbe vyote si sawa. Miili ya binadamu ni ya
namna moja, ya wanyama ni ya namna nyingine, ya ndege ni ya namna nyingine na
miili ya samaki pia ni ya namna nyingine.
40 Iko miili ya mbinguni na miili ya duniani; uzuri wa
miili ya mbinguni ni mwingine, na na uzuri wa miili ya duniani ni mwingine.
41 Uko uzuri wa jua, wa mwezi na wa nyota; hata nyota nazo
huhitilafiana kwa uzuri.
42 Ndivyo ilivyo kuhusu ufufuo wa wafu. Kama vile mbegu,
mwili huzikwa ardhini ukiwa katika hali ya kuharibika, lakini hufufuliwa katika
hali ya kutoharibika.
43 Huzikwa katika hali duni, hufufuliwa katika hali tukufu;
huzikwa katika hali dhaifu, hufufuliwa ukiwa wenye nguvu.
44 Unapozikwa ni mwili wa kawaida, unapofufuliwa ni mwili
wa kiroho. Kuna mwili wa kawaida na kutakuwa na mwili wa kiroho.
45 Maana Maandiko yasema: "Mtu wa kwanza, Adamu,
alikuwa kiumbe mwenye uhai;" lakini adamu wa mwisho ni Roho awapaye watu
uzima.
46 Lakini unaotangulia kuwako si ule mwili wa kiroho, ila
ule mwili wa kawaida kisha ule mwili wa kiroho.
47 Adamu wa kwanza aliumbwa kwa udongo, alitoka ardhini;
mtu wa pili alitoka mbinguni.
48 Wote walio wa dunia wako kama huyo mtu aliyeumbwa kwa
udongo; wale walio wa mbinguni wako kama yule aliyetoka mbinguni.
49 Kama vile tulivyofanana na yule aliyeumbwa kwa udongo,
vivyo hivyo tutafanana na huyohuyo aliyetoka mbinguni.
50 Basi, ndugu, nasema hivi: kile kilichofanywa kwa mwili
na damu hakiwezi kuushiriki Ufalme wa Mungu; na chenye kuharibika hakiwezi kuwa
na hali ya kutoharibika.
51 Sikilizeni, nawaambieni siri: sisi hatutakufa sote, ila
sote tutageuzwa
52 wakati wa mbiu ya mwisho, kwa nukta moja, kufumba na
kufumbua. Maana mbiu itakapolia, wafu watafufuliwa katika hali ya kutoweza kufa
tena, na sisi tutageuzwa.
53 Maana ni lazima kila kiharibikacho kijivalie hali ya
kutoharibika, mwili uwezao kufa ujivalie hali ya kutokufa.
54 Basi, mwili huu wenye kuharibika utakapojivalia hali ya
kutoharibika, na kile chenye kufa kitakapojivalia hali ya kutokufa, hapo ndipo
litakapotimia lile neno lililoandikwa: "Kifo kimeangamizwa ushindi
umekamilika!"
55
"Kifo, ushindi wako uko wapi? Uwezo wako wa kuumiza uko wapi?"
56 Ukali
wa kifo hutokana na dhambi, nayo dhambi hupata nguvu yake katika Sheria.
57 Lakini
tumshukuru Mungu anayetupatia ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.
58 Basi, ndugu zangu wapenzi, simameni imara na thabiti.
Endeleeni daima kuwa na bidii katika kazi ya Bwana, mkijua kwamba kazi
mnayofanya katika utumishi wa Bwana haitapotea bure.
|