Chapter 16
1 Sasa, yahusu ule mchango kwa ajili ya watu wa Mungu:
fanyeni kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia.
2 Kila Jumapili kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha
kadiri ya mapato yake, ili kusiwe na haja ya kufanya mchango wakati
nitakapokuja.
3 Wakati nitakapokuja kwenu, nitawatuma wale mtakaowachagua
miongoni mwenu wapeleke barua na zawadi zenu Yerusalemu.
4 Kama itafaa nami niende, basi, watakwenda pamoja nami.
5 Nitakuja kwenu, baada ya kupitia Makedonia - maana
nataraji kupitia Makedonia.
6 Labda nitakaa kwenu kwa muda fulani, au huenda nitakaa
pamoja nanyi wakati wote wa baridi, ili mpate kunisaidia niendelee na safari
yangu kokote nitakakokwenda.
7 Sipendi kupita kwenu harakaharaka na kuendelea na safari.
Natumaini kukaa kwenu kwa kitambo fulani, Bwana akiniruhusu.
8 Lakini nitabaki hapa Efeso mpaka siku ya Pentekoste.
9 Mlango uko wazi kabisa kwa ajili ya kazi yangu muhimu
hapa, ingawa wapinzani nao ni wengi.
10 Timotheo akija, angalieni asiwe na hofu yoyote wakati
yupo kati yenu, kwani anafanya kazi ya Bwana kama mimi.
11 Kwa hiyo mtu yeyote asimdharau, ila msaidieni aendelee
na safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu, maana mimi namngojea pamoja
na ndugu zetu.
12 Kuhusu ndugu Apolo, nimemsihi sana aje kwenu pamoja na
ndugu wengine, lakini hapendelei kabisa kuja sasa ila atakuja mara
itakapowezekana.
13 Kesheni, simameni imara katika imani, muwe hodari na
wenye nguvu.
14 Kila mfanyacho kifanyike kwa upendo.
15 Ndugu, mnaifahamu jamaa ya Stefana; wao ni watu wa
kwanza kabisa kuipokea imani ya Kikristo katika Akaya, na wamejitolea
kuwatumikia watu wa Mungu. Ninawasihi ninyi ndugu zangu,
16 muufuate uongozi wa watu kama hao, na uongozi wa kila
mtu afanyaye kazi na kutumikia pamoja nao.
17 Nafurahi sana kwamba Stefana, Fortunato na Akaiko
wamefika; wamelijaza pengo lililokuwako kwa kutokuwako kwenu.
18 Wameiburudisha roho yangu na yenu pia. Kwa hiyo inafaa
kuwakumbuka watu wa namna hii.
19 Makanisa yote ya Asia yanawasalimuni. Akula na Priskila
pamoja na watu wote wa Mungu walio nyumbani mwao wanawasalimuni sana katika
Bwana.
20 Ndugu wote wanawasalimuni. Nanyi salimianeni kwa ishara
ya mapendo ya Mungu.
21 Mimi Paulo nawasalimuni, nikiandika kwa mkono wangu
mwenyewe.
22 Yeyote
asiyempenda Bwana, na alaaniwe. MARANA THA - BWANA, njoo!
23 Neema
ya Bwana Yesu iwe nanyi.
24 Mapendo
yangu yawe kwenu katika kuungana na Kristo Yesu.
|