2 Corinthians
Chapter 1
1 Mimi
Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo,
tunawaandikia ninyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho, na watu wote wa Mungu
kila mahali katika Akaya.
2
Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
3 Atukuzwe
Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye
kuleta faraja yote.
4 Yeye
hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine
katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.
5 Naam,
kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi
kufarijiwa naye.
6 Ikiwa
tunapata taabu, basi ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu. Tukifarijika, ni
kwa ajili ya kuwafariji ninyi na kuwaunga mkono mpate nguvu ya kustahimili
mateso yaleyale tunayoteseka sisi.
7 Tena,
matumaini tuliyo nayo kwa ajili yenu ni imara; tunajua kwamba mkishiriki mateso
yetu, mtashiriki pia faraja yetu.
8 Ndugu,
tunataka kuwajulisheni taabu zilizotupata kule Asia; taabu hizo zilitulemea kupita
kiasi, hata tukakata matumaini yote ya kuendelea kuishi.
9 Naam,
tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili
tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu
zetu sisi wenyewe.
10 Yeye
alituokoa katika hatari kubwa ya kifo, na anaendelea kutuokoa; sisi tumemwekea
tumaini letu kwamba atatuokoa tena,
11 ninyi
mkiwa mnatuunga mkono kwa kutuombea. Hivyo neema tutakazokuwa tumepata kutokana
na maombi ya watu wengi hivyo, ziwe sababu ya watu wengi zaidi kumshukuru Mungu
kwa ajili yetu.
12 Sisi
tunajivunia kitu kimoja: dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi
ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na
Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali neema ya Mungu.
13
Tunawaandikia ninyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba
mtaelewa vizuri kabisa,
14 maana
mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile Siku ya Bwana
Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea ninyi fahari.
15 Nikiwa
na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu.
16
Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia, na wakati wa kurudi
pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea.
17 Je,
mnadhani nilipopanga hivyo nimekuwa kama mtu asiye na msimamo? Je, mnadhani
kwamba ninafanya uamuzi wangu kwa fikira za kibinadamu na kwamba nasema
"Ndiyo" na "Siyo" papo hapo?
18 Mungu
ni ukweli mtupu; basi, kile tulichowaambia ninyi si jambo la "Ndiyo"
na "Siyo".
19 Maana
Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silwano na Timotheo, tulimhubiri
kwenu, hakuwa mtu wa "Ndiyo" na "Siyo"; bali yeye daima ni
"Ndiyo" ya Mungu.
20 Maana
ndani yake ahadi zote za Mungu zimekuwa "Ndiyo". Kwa sababu hiyo,
"Amina" yetu husemwa kwa njia ya Kristo kwa ajili ya kumtukuza Mungu.
21 Mungu
mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na ninyi pia katika Kristo, na ndiye
anayetuweka wakfu;
22 ndiye
aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama
dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.
23 Mungu
ndiye shahidi wangu - yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho, kwa
sababu tu ya kuwahurumieni.
24
Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; ninyi mko imara katika imani yenu.
Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu.
|