Chapter 2
1 Basi
nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni.
2 Maana
nikiwahuzunisha ninyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale
niliowahuzunisha!
3 Ndiyo
maana niliwaandikia - sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na ninyi ambao ndio
mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba, mimi nikifurahi, ninyi nyote
pia mnafurahi.
4
Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa
machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha ninyi, bali kwa ajili ya
kuwaonyesheni kwamba nawapenda mno.
5 Ikiwa
kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi - ila amewahuzunisha
ninyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi.
6 Adhabu
aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha.
7
Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije
akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa.
8 Kwa hiyo
nawasihi: mwonyesheni kwamba mnampenda.
9
Madhumuni yangu kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo.
10 Mkimsamehe
mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe - kama kweli ninacho cha kusamehe -
nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu,
11 ili
tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo.
12
Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa
ajili ya kazi ya Bwana.
13 Lakini
nilifadhaika sana kwa kutomkuta ndugu yetu Tito. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda
Makedonia.
14 Lakini,
shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo.
Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali.
15 Maana
sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo
anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote wanaookolewa na wanaopotea.
16 Kwa
wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo
ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo?
17 Sisi si
kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa
unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na
Kristo.
|