Chapter 4
1 Basi,
Mungu, kwa huruma yake, ametukabidhi kazi hii na hivyo hatufi moyo.
2
Tumeyaacha kabisa mambo yote ya aibu na ya kisirisiri. Hatuishi tena kwa
udanganyifu, wala kwa kulipotosha neno la Mungu; bali tunaudhihirisha ukweli
kwa kuufanya ukweli, na hivyo kujiweka chini ya uamuzi wa dhamiri za watu mbele
ya Mungu.
3 Maana, kama Habari Njema tunayohubiri
imefichika, imefichika tu kwa wale wanaopotea.
4 Hao
hawaamini kwa sababu yule mungu wa ulimwengu huu amezitia giza akili zao
wasipate kuuona wazi mwanga wa Habari Njema ya utukufu wa Kristo, ambaye ni
mfano kamili wa Mungu.
5 Maana
hatujitangazi sisi wenyewe, ila tunamhubiri Yesu Kristo aliye Bwana, sisi
wenyewe tukiwa watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.
6 Mungu
ambaye alisema, "Mwanga na uangaze kutoka gizani," ndiye mwenye
kuiangaza mioyo yetu, na kutupatia mwanga wa ujuzi wa utukufu wa Mungu uangazao
katika uso wa Kristo.
7 Basi,
sisi tulio na hazina hii tuko tu kama vyombo vya udongo, ili ionekane wazi
kwamba nguvu hiyo kuu yatoka kwa Mungu wala si kwetu sisi wenyewe.
8 Daima
twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa;
9
twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini,
hatukuangamizwa.
10 Kila
wakati tumekuwa tukichukua mwilini mwetu kifo cha Kristo, ili uhai wake Yesu
pia udhihirike katika miili yetu.
11 Naam,
katika maisha yetu yote tunakabiliwa na kifo daima kwa ajili ya Yesu, ili uzima
wake Yesu udhihirike katika miili yetu inayokufa.
12 Hii ina
maana kwamba ndani yetu kifo kinafanya kazi, lakini ndani yenu uhai unafanya
kazi.
13
Maandiko Matakatifu yasema: "Niliamini, ndiyo maana nilinena." Nasi
pia, tukiwa na moyo huohuo wa imani, tunaamini, na kwa sababu hiyo twanena.
14 Tunajua
kwamba yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na
kutuweka mbele yake pamoja nanyi.
15 Yote
haya ni kwa faida yenu; ili kama vile neema ya Mungu inavyoenea kwa watu wengi
zaidi na zaidi vivyo hivyo watu wengi zaidi watoe shukrani nyingi kwa utukufu
wa Mungu.
16 Kwa
sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa
ndani tunafanywa wapya siku kwa siku.
17 Taabu
tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu: lakini itatupatia utukufu upitao
matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho.
18 Hivyo
tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana
vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele.
|