Chapter 5
1 Maana
tunajua kwamba hema hii ambayo ndani yake tunaishi sasa hapa duniani, yaani mwili
wetu, itakapong`olewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele
isiyotengenezwa kwa mikono.
2 Na sasa,
katika hali hii, tunaugua, tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo
mbinguni.
3 Naam, tunapaswa
kuvikwa namna hiyo ili tusije tukasimama mbele ya Mungu bila vazi.
4 Tukiwa
bado katika hema hii ya duniani, tunalia kwa kukandamizwa; si kwamba tunataka
kuuvua mwili huu wa kufa, ila tuna hamu ya kuvalishwa ule usiokufa, ili kile
chenye kufa kimezwe kabisa na uhai.
5 Mungu
mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya
yote aliyotuwekea.
6 Tuko
imara daima. Tunajua kwamba kuishi katika mwili huu tu ni kukaa mbali na Bwana.
7 Maana tunaishi kwa imani, na si kwa kuona.
8 Lakini tuko imara na tungependelea hata kuyahama makao
haya, tukahamie kwa Bwana.
9 Lakini jambo la maana zaidi, tunataka kumpendeza, iwe
tunaishi hapa duniani au huko.
10 Maana sote ni lazima tusimame mbele ya kiti cha hukumu
cha Kristo, ili kila mmoja apokee anayostahili kwa matendo aliyoyafanya wakati
alipokuwa anaishi duniani, mema au mabaya.
11 Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo
tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba
nanyi pia mnatujua kinaganaga.
12 Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila
tunataka kuwapa ninyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu
wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni.
13 Ikiwa tumeonekana kuwa wendawazimu, hiyo ni kwa ajili ya
Mungu; na ikiwa tunazo akili zetu timamu, hiyo ni kwa faida yenu.
14 Maana mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao
tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana
kwamba wote wanashiriki kifo chake.
15 Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi
kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa
ajili yao.
16 Basi, tangu sasa, sisi hatumpimi mtu yeyote kibinadamu.
Hata kama kwa wakati mmoja tulimpima Kristo kibinadamu, sasa si hivyo tena.
17 Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo
ya kale yamepita, hali mpya imefika.
18 Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa
njia ya Kristo, akatupa nasi jukumu la kuwapatanisha watu naye.
19 Ndiyo kusema: Mungu, amekuwa akiupatanisha ulimwengu
naye kwa njia ya Kristo, bila kutia maanani dhambi zao binadamu. Yeye ametupa
ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye.
20 Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye Mungu mwenyewe
anatutumia sisi kuwasihi ninyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe
na Mungu.
21 Kristo hakuwa na dhambi, lakini Mungu alimfanya ahusike
na dhambi kwa ajili yetu, ili sisi kwa kuungana naye, tupate kuushiriki
uadilifu wake Mungu.
|