Chapter 7
1 Basi, wapenzi wangu, tukiwa tumepewa ahadi hizi zote, na
tujitakase na chochote kiwezacho kuchafua miili na roho zetu, tuwe watakatifu
kabisa, na tuishi kwa kumcha Mungu.
2 Tunaomba mtupe nafasi mioyoni mwenu! Hatujamkosea mtu
yeyote, hatujamdhuru wala kumdanganya mtu yeyote.
3 Sisemi mambo haya kwa ajili ya kumhukumu mtu; maana, kama
nilivyokwisha sema, ninyi mko mioyoni mwetu, tufe pamoja, tuishi pamoja.
4 Nina imani kubwa sana ninaposema nanyi; naona fahari
kubwa juu yenu! Katika taabu zetu nimepata kitulizo kikubwa na kufurahi mno.
5 Hata baada ya kufika Makedonia hatukuweza kupumzika. Kila
upande tulikabiliwa na taabu: nje ugomvi; ndani hofu.
6 Lakini Mungu, mwenye kuwapa shime wanyonge alitupa moyo
sisi pia kwa kuja kwake Tito.
7 Si tu kwa kule kuja kwake Tito, bali pia kwa sababu ya
moyo mliompa ninyi. Yeye ametuarifu jinsi mnavyotamani kuniona, jinsi mlivyo na
huzuni, na mnavyotaka kunitetea. Jambo hili linanifurahisha sana.
8 Maana, hata kama kwa barua ile yangu nimewahuzunisha,
sioni sababu ya kujuta. Naam, naona kwamba barua hiyo iliwatia huzuni lakini
kwa muda.
9 Sasa nafurahi, si kwa sababu mmehuzunika, ila kwa kuwa
huzuni yenu imewafanya mbadili nia zenu na kutubu. Mmehuzunishwa kadiri ya
mpango wa Mungu, na kwa sababu hiyo hatukuwadhuru ninyi kwa vyovyote.
10 Kuwa na huzuni jinsi atakavyo Mungu, husababisha
badiliko la moyo, badiliko lenye kuleta wokovu; hivyo hakuna sababu ya kujuta.
Lakini huzuni ya kidunia huleta kifo.
11 Sasa mnaweza kuona matokeo ya kuona huzuni jinsi Mungu
atakavyo: ninyi mmepata kuwa sasa watu wenye jitihada, wenye hoja, mnashtuka na
kuogopa, mna bidii na mko tayari kuona kwamba haki yatekelezwa. Ninyi
mmethibitisha kwa kila njia kwamba hamna hatia kuhusu jambo hili.
12 Hivyo, ingawa niliandika ile barua, haikuwa kwa ajili ya
yule aliyekosa, au kwa ajili ya yule aliyekosewa. Niliandika kusudi ionekane
wazi mbele ya Mungu jinsi mlivyo na bidii kwa ajili yetu.
13 Ndiyo maana sisi tulifarijika sana. Siyo kwamba
tulifarijika tu, ila pia Tito alitufurahisha kwa furaha aliyokuwa nayo kutokana
na jinsi mlivyomchangamsha moyo.
14 Mimi nimewasifu sana mbele yake, na katika jambo hilo
sikudanganyika. Tumewaambieni ukweli daima, na kule kuwasifia ninyi mbele ya
Tito kumekuwa jambo la ukweli mtupu.
15 Hivyo upendo wake wa moyo kwenu unaongezeka zaidi
akikumbuka jinsi ninyi nyote mlivyo tayari kutii, na jinsi mlivyomkaribisha kwa
hofu nyingi na kutetemeka.
16 Nafurahi sana kwamba naweza kuwategemea ninyi kabisa
katika kila jambo.
|