Chapter 9
1 Si lazima kuandika zaidi kuhusu huduma hiyo yenu kwa
ajili ya watu wa Mungu.
2 Ninajua jinsi mlivyo na moyo wa kusaidia, na nilijivuna
juu yenu kuhusu jambo hilo mbele ya watu wa Makedonia. Niliwaambia: "Ndugu
zetu wa Akaya wako tayari tangu mwaka jana." Hivyo, moto wenu umekwisha
wahimiza watu wengi zaidi.
3 Basi, nimewatuma ndugu zetu hao, ili fahari yetu juu yenu
ionekane kwamba si maneno matupu, na kwamba mko tayari kabisa na msaada wenu
kama nilivyosema.
4 Isije ikawa kwamba watu wa Makedonia watakapokuja pamoja
nami tukawakuta hamko tayari, hapo sisi tutaaibika - bila kutaja aibu
mtakayopata ninyi wenyewe - kwa sababu tutakuwa tumewatumainia kupita kiasi.
5 Kwa hiyo, nimeona ni lazima kuwaomba hawa ndugu watutangulie
kuja kwenu, wapate kuweka tayari zawadi yenu kubwa mliyoahidi; nayo ionyeshe
kweli kwamba ni zawadi iliyotolewa kwa hiari na si kwa kulazimishwa.
6 Kumbukeni: "Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye
kwa wingi huvuna kwa wingi."
7 Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na
wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa
kwa furaha.
8 Mungu anaweza kuwapeni ninyi zaidi ya yale mnayoyahitaji,
mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila
kazi njema.
9 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Yeye hutoa kwa
ukarimu, huwapa maskini, wema wahudumu milele."
10 Na Mungu ampaye mkulima mbegu na mkate kwa chakula,
atawapa ninyi pia mbegu mnazohitaji, na atazifanya ziote, ziwe na kuwapa mavuno
mengi ya ukarimu wenu.
11 Yeye atawatajirisha ninyi daima kwa kila kitu, ili watu
wapate kumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi zenu wanazozipokea kwa mikono yetu.
12 Maana huduma hii takatifu mnayoifanya si tu kwamba
itasaidia mahitaji ya watu wa Mungu, bali pia itasababisha watu wengi
wamshukuru Mungu.
13 Kutokana na uthibitisho unaoonyeshwa kwa huduma hii
yetu, watu watamtukuza Mungu kwa sababu ya uaminifu wenu kwa Habari Njema ya
Kristo mnayoiungama, na pia kwa sababu ya ukarimu mnaowapa wao na watu wote.
14 Kwa hiyo watawaombea ninyi kwa moyo kwa sababu ya neema
ya pekee aliyowajalieni Mungu.
15 Tumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi yake isiyo na
kifani!
|