Chapter 10
1 Mimi Paulo mwenyewe ambaye naonekana kuwa mpole nikiwa
pamoja nanyi, lakini mkali wakati nikiwa mbali nanyi, nawasihini kwa huruma na
wema wake Kristo.
2 Nawaombeni msinisababishe kuwa mkali wakati nitakapokuja,
maana nina hakika naweza kuwa mkali kwa wote wale wanaotudhania kwamba tunaishi
kidunia.
3 Kweli tunaishi duniani, lakini hatupigani vita kidunia.
4 Maana, silaha tunazotumia katika vita vyetu si silaha za
kidunia, ila ni nguvu za Mungu zenye kuharibu ngome zote. Tunaharibu hoja zote
za uongo,
5 na kubomoa kila kizuizi cha majivuno kilichowekwa
kuipinga elimu ya Mungu; tunaziteka fikira zote na kuzifanya zimtii Kristo.
6 Mkisha kuwa wakamilifu katika kutii, sisi tuko tayari
kuadhibu kila namna ya kutotii.
7 Ninyi
hutazama mambo kwa nje tu. Je, yupo mtu yeyote anayedhani kwamba yeye ni wa
Kristo? Sawa! Basi, afikirie vilevile kwamba sisi pia ni wa Kristo kama yeye
alivyo wa Kristo.
8 Hata
kama nimezidi katika kujivuna kwangu juu ya ule uwezo aliotupa - uwezo wa
kuwajenga na sio wa kubomoa - hata hivyo sijutii hata kidogo.
9 Sipendi
mfikiri kwamba nataka kuwatisha ninyi kwa barua zangu.
10 Mtu
anaweza kusema: "Barua za Paulo ni kali na zenye maneno mazito, lakini
yeye mwenyewe anapokuwa pamoja nasi ni mtu dhaifu, na hata anapoongea maneno
yake ni kama si kitu."
11 Mtu
asemaye hivyo heri akumbuke kwamba hakuna tofauti ya yale tunayoandika katika
barua wakati tuko mbali, na yale tutakayofanya wakati tutakapokuwa nanyi.
12 Kwa
vyovyote hatungethubutu kujiweka au kujilinganisha na wale watu wanaojisifia
wenyewe. Watu wenye kujifanya wao kuwa kipimo cha kujipimia, na watu
wanaojilinganisha wenyewe kwa wenyewe, ni wapumbavu.
13 Lakini
sisi hatutajivuna kupita kiasi; kujivuna huko kutabaki katika kile kipimo cha
kazi aliyotukabidhi Mungu, kazi ambayo tunaifanya pia kwenu.
14 Na kwa
vile ninyi mu katika mipaka hiyo, hatukuipita tulipokuja kwenu, tukiwaleteeni
Habari Njema juu ya Kristo.
15 Basi,
hatujivunii kazi waliyofanya wengine zaidi ya kipimo tulichopewa; ila
tunatumaini kwamba imani yenu itazidi miongoni mwenu kufuatana na kipimo
alichotuwekea Mungu.
16 Hapo
tutaweza kuihubiri Habari Njema katika nchi nyingine, mbali nanyi; na haitakuwa
shauri la kujivunia kazi waliyofanya watu wengine mahali pengine.
17 Lakini
kama yasemavyo Maandiko: "Mwenye kuona fahari na aone fahari juu ya
alichofanya Bwana."
18
Anayekubaliwa si yule anayejisifu mwenyewe, bali yule anayesifiwa na Bwana.
|