Chapter 13
1 Hii ni mara yangu ya tatu kuja kwenu. "Kila tatizo
litatatuliwa kwa ushahidi wa watu wawili au watatu," yasema Maandiko.
2 Nilikwisha sema, na kama ilivyokuwa safari ya pili, sasa
nasema tena nikiwa mbali: wale wote waliotenda uovu bila kutubu, na pia wale
wengine, nitakapokuja, watakiona cha mtema kuni.
3 Mtajionea wenyewe kwamba Kristo anasema ndani yangu.
Kwenu Kristo si dhaifu; bali nguvu yake yafanya kazi miongoni mwenu.
4 Maana hata kama alisulubiwa kwa sababu ya udhaifu, lakini
sasa anaishi kwa uwezo wa Mungu. Sisi pia tu dhaifu kwa kuungana naye lakini
tutaishi naye kwa uwezo wa Mungu kwa ajili yenu.
5 Jichunguzeni ninyi wenyewe mpate kujua kama kweli mnayo
imani. Jichunguzeni ninyi wenyewe. Je, hamjui kwamba Kristo Yesu yumo ndani
yenu? Kama sivyo, basi ninyi mmeshindwa.
6 Lakini natumaini kwamba ninyi mnajua kuwa sisi
hatukushindwa.
7 Tunamwomba Mungu msifanye uovu wowote, lakini si kusudi
tuonekane kama watu waliokwisha faulu, bali mpate kutenda mema, hata kama sisi
tunaonekana kuwa tumeshindwa.
8 Maana hatuwezi kuupinga ukweli; uwezo tulio nao ni wa
kuuendeleza ukweli.
9 Tunafurahi kwamba sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu;
kwa hiyo tunaomba mpate kuwa wakamilifu.
10 Basi, ninaandika barua hii nikiwa mbali, ili
nitakapofika kwenu nisilazimike kuwa mkali kwenu kwa kutumia ule uwezo alionipa
Bwana; naam, uwezo wa kujenga na si wa kubomoa.
11 Kwa sasa, ndugu, kwaherini! Muwe na ukamilifu, shikeni
mashauri yangu, muwe na nia moja; kaeni kwa amani. Naye Mungu wa mapendo na
amani atakuwa pamoja nanyi.
12 Salimianeni kwa ishara ya upendo. Watu wote wa Mungu
huku wanawasalimuni.
13 Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na umoja
wa Roho Mtakatifu, viwe nanyi nyote.
|