Galatians
Chapter 1
1 Mimi
Paulo mtume,
2 na ndugu
wote walio pamoja nami, tunayaandikia makanisa yaliyoko Galatia. Mimi nimepata
kuwa mtume si kutokana na mamlaka ya binadamu, wala si kwa nguvu ya mtu, bali
kwa uwezo wa Yesu Kristo na wa Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka wafu.
3 Tunawatakieni
neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.
4 Kristo
alijitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na mapenzi ya Mungu wetu
na Baba, ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu mbaya wa sasa.
5 Kwake
yeye uwe utukufu milele! Amina.
6
Nashangaa kwamba muda mfupi tu umepita, nanyi mnamwasi yule aliyewaita kwa
neema ya Kristo, mkafuata Habari Njema ya namna nyingine.
7 Lakini hakuna "Habari Njema" nyingine. Ukweli
ni kwamba wako watu wanaowavurugeni, watu wanaotaka kuipotosha Habari Njema ya
Kristo.
8 Lakini, hata kama mmoja wetu au malaika kutoka mbinguni,
atawahubirieni Habari Njema tofauti na ile tuliyowahubirieni sisi, basi huyo na
alaaniwe!
9 Tulikwisha sema, na sasa nasema tena: kama mtu yeyote
anawahubirieni Habari Njema ya aina nyingine, tofauti na ile mliyokwisha pokea,
huyo na alaaniwe!
10 Sasa nataka kibali cha nani: cha binadamu, ama cha
Mungu? Au je, nataka kuwapendeza watu? Kama ningefanya hivyo, mimi singekuwa
kamwe mtumishi wa Kristo.
11 Ndugu, napenda mfahamu kwamba ile Habari Njema
niliyoihubiri si ujumbe wa kibinadamu.
12 Wala mimi sikuipokea kutoka kwa binadamu, wala
sikufundishwa na mtu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia.
13 Bila shaka mlikwisha sikia jinsi nilivyokuwa ninaishi
zamani kwa kuzingatia dini ya Kiyahudi, na jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu
kupita kiasi na kutaka kuliharibu kabisa.
14 Naam, mimi niliwashinda wengi wa wananchi wenzangu wa
rika langu katika kuizingatia dini ya Kiyahudi, nikajitahidi sana kuyashika
mapokeo ya wazee wetu.
15 Lakini Mungu, kwa neema yake, alikuwa ameniteua hata
kabla sijazaliwa, akaniita nimtumikie.
16 Mara tu alipoamua kunifunulia Mwanae kusudi niihubiri
Habari Njema yake kwa watu wa mataifa mengine, bila kutafuta maoni ya binadamu,
17 na bila kwenda kwanza Yerusalemu kwa wale waliopata kuwa
mitume kabla yangu, nilikwenda kwanza Arabia, kisha nikarudi tena Damasko.
18 Ilikuwa tu baada ya miaka mitatu, ndipo nilipokwenda
Yerusalemu kuonana na Kefa; nilikaa kwake siku kumi na tano.
19 Lakini sikuwaona mitume wengine isipokuwa Yakobo, ndugu
yake Bwana.
20 Haya ninayowaandikieni, Mungu anajua; sisemi uongo.
21 Baadaye nilikwenda katika tarafa za Siria na Kilikia.
22 Wakati huo, mimi binafsi sikujulikana kwa jumuiya za
Wakristo kule Yudea.
23 Walichokuwa wanajua ni kile tu walichosikia: "Mtu
yule aliyekuwa akitutesa hapo awali, sasa anaihubiri imani ileile aliyokuwa
anajaribu kuiangamiza."
24 Basi, wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.
|