Chapter 3
1 Enyi Wagalatia, mmekuwa wajinga kweli! Ni nani
aliyewaloga? Habari juu ya kusulubiwa kwake Yesu Kristo ilielezwa waziwazi
mbele ya macho yenu.
2 Napenda kujua tu kitu kimoja kutoka kwenu: Je, mlipokea
Roho wa Mungu kwa sababu ya kutimiza matakwa ya Sheria ama kwa sababu ya
kuisikia na kuiamini Habari Njema?
3 Je, mu wajinga
kiasi hicho? Ninyi mlianza yote kwa msaada wa Roho je, mnataka sasa kumaliza
kwa nguvu zenu wenyewe?
4 Je, mambo yale
yote yaliyowapata ninyi yamekuwa bure tu? Haiwezekani!
5 Je, Mungu
huwajalia Roho na kutenda miujiza kati yenu ati kwa sababu mnatimiza
yanayotakiwa na sheria, ama kwa sababu mnasikia Habari Njema na kuiamini?
6 Chukueni kwa
mfano habari za Abrahamu: yeye alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa
mwadilifu.
7 Sasa basi
jueni kwamba watu wenye kumwamini ndio walio watoto halisi wa Abrahamu.
8 Maandiko
Matakatifu yalionyesha kabla kwamba Mungu atawakubali watu wa mataifa kuwa
waadilifu kwa njia ya imani. Hivyo Maandiko Matakatifu yalitangulia kumtangazia
Abrahamu Habari Njema: "Katika wewe mataifa yote yatabarikiwa."
9 Basi, wale
walio na imani wanabarikiwa pamoja na Abrahamu aliyeamini.
10 Lakini wote
wanaotegemea tu kutimiza yanayotakiwa na Sheria, wako chini ya laana. Maana,
Maandiko Matakatifu yasema: "Yeyote asiyeshika na kutimiza yote
yaliyoandikwa katika kitabu cha Sheria, yuko chini ya laana."
11 Ni dhahiri
kwamba Sheria haiwezi kumfanya mtu akubaliwe kuwa mwadilifu; maana Maandiko
Matakatifu yasema: "Mwadilifu kwa imani ataishi."
12 Lakini Sheria
haitegemei imani, ila Maandiko yasema: "Mwenye kutimiza yanayotakiwa na
Sheria ataishi."
13 Kristo
alitukomboa kutoka katika laana ya Sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili
yetu; maana Maandiko yanasema: "Yeyote aliyetundikwa msalabani
amelaaniwa."
14 Jambo hili
lilifanyika kusudi ile baraka aliyopewa Abrahamu iwashukie watu wa mataifa
mengine kwa njia ya Kristo, na ili kwa imani, tumpokee yule Roho ambaye Mungu
alituahidia.
15 Ndugu,
nitawapeni mfano kutoka maisha yetu ya kila siku. Fikirini juu ya mkataba kati
ya watu wawili. Mkataba ukisha fanyika na kutiwa sahihi hapana mtu anayeuweka
kando au kuuongezea kitu.
16 Basi,
Abrahamu alipewa ahadi, yeye pamoja na mzawa wake. Maandiko hayasemi: "Na
wazawa wake," yaani wengi, bali yasema, "Na mzawa wake," yaani
mmoja, naye ndiye Kristo.
17 Ninachotaka
kusema ni hiki: Mungu alifanya agano lake akalithibitisha; Sheria ambayo
ilitokea miaka mia nne na thelathini baadaye, haiwezi kulitangua hilo agano
wala kuibatilisha hiyo ahadi.
18 Maana, kama
urithi ya Mungu inategemea Sheria, basi, haiwezi kutegemea tena ahadi ya Mungu.
Kumbe, lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa sababu aliahidi.
19 Ya nini basi,
Sheria? Iliongezwa hapo ili kuonyesha uhalifu ni kitu gani, mpaka atakapokuja
yule mzawa wa Abrahamu aliyepewa ile ahadi. Sheria ililetwa na malaika kwa
mkono wa mpatanishi.
20 Ama hakika,
mpatanishi hahitajiwi ikiwa jambo lenyewe lamhusu mtu mmoja; na Mungu ni mmoja.
21 Je, Sheria
inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria
ambayo ingeweza kuwapa watu uzima, basi, tungeweza kukubaliwa kuwa waadilifu
kwa njia ya Sheria.
22 Lakini sivyo;
Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala
wa dhambi; na hivyo, kwa kumwamini Yesu Kristo, wenye kuamini watimiziwe ile
ahadi.
23 Kabla ya
kujaliwa imani, Sheria ilitufanya wafungwa mpaka imani hiyo iliyokuwa inakuja
ifunuliwe.
24 Basi, hiyo
Sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya imani,
tukubaliwe kuwa waadilifu.
25 Tangu kufika
kwa hiyo imani, Sheria si mlezi wetu tena.
26 Kwa njia ya
imani, ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika kuungana na Kristo.
27 Ninyi nyote
mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo.
28 Hivyo, hakuna
tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na
mwanamke. Nyote ni kitu kimoja katika kuungana na Kristo Yesu.
29 Ikiwa ninyi
ni wa Kristo, basi ni wazawa wa Abrahamu, na mtapokea yale aliyoahidi Mungu.
|