Chapter 4
1 Basi, nasema hivi:
mrithi, akiwa bado mtoto, hawi tofauti na mtumwa ingawaje mali yote ni yake.
2 Wakati huo
wote yuko chini ya walezi na wadhamini mpaka wakati ule uliowekwa na baba yake.
3 Hali kadhalika
na sisi tulipokuwa bado watoto, tulikuwa watumwa wa pepo watawala wa ulimwengu.
4 Lakini wakati
ule maalumu ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanawe aliyezaliwa na mwanamke, akaishi
chini ya Sheria
5 apate
kuwakomboa wale waliokuwa chini ya Sheria ili sisi tufanywe wana wa Mungu.
6 Kwa vile sasa
ninyi ni wana, Mungu amemtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwenu, Roho ambaye hulia
"Aba," yaani "Baba."
7 Basi, wewe si mtumwa tena, bali mwana. Na ikiwa ni mwana,
basi, wewe utapokea yote Mungu aliyowawekea watoto wake.
8 Zamani hamkumjua Mungu na hivyo mkatumikia miungu isiyo
miungu kweli.
9 Lakini sasa, kwa vile mnamjua Mungu, au tuseme
mnajulikana na Mungu, mnawezaje tena kurudi kwa wale pepo maskini na dhaifu
hata kutaka kuwatumikia tena?
10 Bado
mnaadhimisha siku, miezi na miaka!
11 Nahofu
kwamba labda kazi niliyoifanya kwa ajili yenu imepotea bure!
12 Ndugu,
nawasihi muwe kama mimi, kwa vile hata mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea
ubaya wowote.
13 Mnajua
kwamba ugonjwa wangu ndio ulionipatia fursa ya kuwahubirieni Habari Njema kwa
mara ya kwanza.
14 Hata
hivyo, wakati ule hamkunidharau wala kunikataa kwa sababu ya udhaifu wangu
ingawa mlishawishiwa kufanya hivyo; lakini mlinipokea kama malaika wa Mungu,
kama vile ningekuwa Kristo Yesu mwenyewe.
15 Mlikuwa
wenye furaha; sasa kumetokea nini? Naapa kwamba wakati ule mngaliweza hata
kuyang`oa macho yenu na kunipa mimi.
16 Je,
sasa nimekuwa adui yenu kwa sababu ya kuwaambieni ukweli?
17 Hao
watu wengine wanawahangaikia ninyi, lakini nia zao si njema. Wanataka
kuwatenganisha nami ili ninyi muwahangaikie wao.
18 Kwa
kweli ni jambo jema daima kuwahangaikia wengine katika mambo mema, na si tu
wakati mimi nipo pamoja nanyi.
19 Watoto
wangu, kama vile mama mja mzito anavyotaabika wakati wa kujifungua, mimi
nataabika tena kwa ajili yenu mpaka hapo hali yake Kristo itakapoundwa ndani
yenu.
20 Laiti
ningekuwa pamoja nanyi sasa, maana ningalipata msimamo ufaao juu yenu! Nina
wasiwasi sana nanyi!
21
Niambieni, enyi mnaopenda kutawaliwa na sheria: Je, mnasikia isemavyo Sheria?
22
Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Abrahamu alikuwa na watoto wawili:
mmoja kwa mwanamke mtumwa, na wa pili kwa mwanamke huru.
23 Yule wa
mwanamke mtumwa alizaliwa kama kawaida, lakini yule wa mwanamke huru alizaliwa
kutokana na ahadi ya Mungu.
24 Mambo
hayo yamekuwa mfano; mama hao wawili ni mfano wa maagano mawili; la kwanza ni
lile lililofanyika mlimani Sinai, mwakilishi wake ni Hagari, na watoto wake
wanazaliwa utumwani.
25 Hagari
anawakilisha mlima Sinai ulioko Arabia, na ni mfano wa Yerusalemu ya sasa, ulio
mtumwa pamoja na watoto wake.
26 Lakini
Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu.
27 Maana
imeandikwa: "Furahi, ewe uliye tasa usiyezaa; paaza sauti wewe usiyepata
kujifungua mtoto; maana watoto wa yule aliyeachwa ni wengi zaidi kuliko wa yule
aliye na mume."
28 Sasa,
basi, ndugu zangu, ninyi ni watoto wa Mungu kutokana na ahadi yake kama
alivyokuwa Isaka.
29 Lakini
kama vile siku zile yule mtoto aliyezaliwa kwa njia ya kawaida alimdhulumu yule
aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho wa Mungu, vivyo hivyo na siku hizi.
30 Lakini
Maandiko Matakatifu yasemaje? Yasema: "Mfukuze mama mtumwa pamoja na
mwanawe; maana mtoto wa mtumwa hatarithi pamoja na mtoto wa mama huru."
31 Kwa
hiyo, basi, ndugu, sisi si watoto wa mtumwa bali wa mama huru.
|