Chapter 6
1 Ndugu,
kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, ninyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu
huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije
nanyi wenyewe mkajaribiwa.
2
Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo.
3 Mtu
akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe.
4 Lakini
kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza
kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu
mwingine.
5 Maana
kila mmoja anao mzigo wake mwenyewe wa kubeba.
6 Mwenye
kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake.
7
Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna.
8 Apandaye
katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho,
atavuna kutoka kwa Roho uzima wa milele.
9 Basi,
tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake.
10 Kwa
hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani
yetu.
11 Tazameni
jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe.
12 Wale
wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha
ninyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: kusudi wao wenyewe wasije
wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo.
13 Maana,
hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki Sheria; huwataka ninyi mtahiriwe wapate
kujivunia alama hiyo mwilini mwenu.
14 Lakini
mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo;
maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa
kwa ulimwengu.
15
Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya.
16
Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli
- Wateule wa Mungu.
17 Basi,
sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni
zile za Yesu.
18 Ndugu,
nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Kristo. Amina.
|