Ephesians
Chapter 1
1 Mimi
Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, nawaandikia ninyi watu wa
Mungu huko Efeso, mlio waaminifu katika kuungana na Kristo Yesu.
2
Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
3 Atukuzwe
Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo
ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni.
4 Kabla ya
kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe
watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake,
5 Mungu
alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu
Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia.
6 Basi,
tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu katika Mwanae mpenzi!
7 Maana
kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo
ulivyo ukuu wa neema yake
8
aliotukirimia bila kipimo! Kwa hekima na ujuzi wake wote
9 Mungu
alitekeleza kile alichonuia, akatujulisha mpango wake uliofichika, ambao
alikuwa ameazimia kuutekeleza kwa njia ya Kristo.
10 Mpango
huo ambao angeutimiza wakati utimiapo ni kukusanya pamoja viumbe vyote, kila
kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo.
11 Kila
kitu hufanywa kufuatana na mpango na uamuzi wa Mungu; naye Mungu ametuteua sisi
tuwe watu wake kwa mapenzi yake katika kuungana na Kristo, kufuatana na azimio
alilofanya tangu mwanzo.
12 Basi,
sisi tuliotangulia kumtumainia Kristo tunapaswa kuusifu utukufu wa Mungu!
13 Nanyi
pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema
iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonyesha kuwa ninyi ni
wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia.
14 Huyu
Roho ni dhamana ya kurithi yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo
hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu
utukufu wake!
15 Kwa
sababu hiyo, tangu niliposikia juu ya imani yenu kwa Bwana Yesu na mapendo yenu
kwa watu wa Mungu,
16
sijaacha kamwe kumshukuru Mungu kwa ajili yenu. Ninawakumbuka katika sala zangu
17 ili
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo Baba mtukufu, awajalieni Roho wake atakayewapa
hekima na kuwafunulieni Mungu mpate kumjua.
18
Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile
tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake,
19 mpate
kutambua jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Uwezo
huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na nguvu ile kuu mno
20
aliyomfufua nayo Kristo kutoka wafu, akamketisha kulia kwake mbinguni.
21 Huko,
Kristo anatawala juu ya kila tawala, mamlaka, enzi na ukuu; anatawala juu ya
kila cheo kiwezacho kutajwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ujao.
22 Mungu
ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa kanisa akiwa mkuu wa
vitu vyote.
23 Kanisa
ni mwili wa Kristo, na ukamilifu wake yeye anayekamilisha vitu vyote kila
mahali.
|