Chapter 4
1 Basi, mimi niliye mfungwa kwa kuwa namtumikia Bwana,
nawasihi muishi maisha yanayostahili wito mlioitiwa.
2 Muwe daima wanyenyekevu, wapole na wenye saburi;
vumilianeni ninyi kwa ninyi kwa mapendo.
3 Fanyeni bidii ya kuhifadhi umoja uletwao na Roho kwa
kuzingatia amani iliyo kati yenu.
4 Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile tumaini
mliloitiwa na Mungu ni moja.
5 Kuna
Bwana mmoja, imani moja na ubatizo mmoja;
6 kuna
Mungu mmoja na Baba wa wote, ambaye yuko juu ya wote, afanya kazi katika yote
na yuko katika yote.
7 Kila
mmoja wetu amepewa neema kadiri ya kipimo alichojaliwa na Kristo.
8 Kama
yasemavyo Maandiko: "Alipopaa mbinguni juu kabisa, alichukua mateka;
aliwapa watu zawadi."
9 Basi, inaposemwa: "alipaa juu," ina maana gani?
Maana yake ni kwamba, kwanza alishuka mpaka chini kabisa duniani.
10 Basi, huyo aliyeshuka hapa duniani, ndiye aliyepaa juu
ya mbingu zote apate kuujaza ulimwengu.
11 Ndiye aliyewapa watu zawadi: wengine aliwajalia wawe
mitume, wengine manabii, wengine wawe waeneza Habari Njema, wengine wachungaji
na walimu.
12 Alifanya hivyo apate kuwatayarisha watu wote wa Mungu
kwa ajili ya kazi ya huduma ya Kikristo ili kuujenga mwili wa Kristo,
13 na hivyo sote tuufikie umoja wa imani na kumjua Mwana wa
Mungu; tuwe watu waliokomaa na kuufikia utimilifu wake Kristo mwenyewe.
14 Basi, hatutakuwa tena kama watoto, tukitupwa na
kupeperushwa huko na huko kwa kila upepo wa mafundisho wanayozua watu
wadanganyifu, ili wawapotoshe wengine kwa hila.
15 Ila, sisi tukisema ukweli kwa moyo wa mapendo tutakua
zidi katika kila jambo kulingana na Kristo ambaye ndiye kichwa;
16 chini ya uongozi wake, viungo vyote vya mwili
hushikamana pamoja, na mwili wote hutegemezwa kwa msaada wa viungo vyake. Basi,
kila kiungo kikitekeleza kazi yake ipasavyo, mwili wote hukua na kujijenga
katika upendo.
17 Basi, kwa jina la Bwana, nawaonyeni: msiishi tena kama
watu wasiomjua Mungu, ambao fikira zao zimekuwa upuuzi mtupu,
18 na
akili zao zimo gizani. Wako mbali na uzima wa Mungu, kwa sababu ya upumbavu
ulio ndani yao na ukaidi wao.
19
Wamepotoka na hawana aibu, wamejitosa katika ufisadi; hufanya kwa pupa kila
aina ya mambo ya aibu.
20 Lakini
ninyi hamkujifunza hivyo juu ya Kristo.
21 Ni
dhahiri kwamba mlisikia barabara habari zake, na mkiwa wafuasi wake
mkafundishwa ukweli ulivyo katika Yesu.
22 Basi,
acheni mwenendo wenu wa awali, yaani ule utu wenu wa kale uliokuwa unaangamizwa
kwa tamaa zake danganyifu.
23
Jirekebisheni upya rohoni na katika fikira zenu.
24 Vaeni
hali mpya ya utu ambayo imeumbwa kwa mfano wa Mungu na ambayo hujionyesha
katika maisha ya kweli ya uadilifu na utakatifu.
25 Kwa hiyo, acheni uongo. Kila mmoja anapaswa kumwambia
mwenzake ukweli, maana kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo.
26 Kama mkikasirika, msikubali hasira yenu iwafanye mtende
dhambi, na wala msikae na hasira kutwa nzima.
27 Msimpe Ibilisi nafasi.
28 Aliyekuwa akiiba, asiibe tena, bali na aanze kufanya
kazi njema kwa mikono yake, apate kuwa na kitu cha kumsaidia mtu aliye maskini.
29 Maneno mabaya hata yasisikike kamwe miongoni mwenu; kila
mara maneno yenu yawe ya kufaa na ambayo hujenga na kuwasaidia wengine, ili
yawaneemeshe wasikilizaji wenu.
30 Msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu maana Roho huyo ni
alama ya Mungu kwenu kwamba ninyi ni watu wake, na thibitisho kwamba siku
itakuja ambapo Mungu atawakomboeni.
31 Basi, achaneni na uhasama, chuki, hasira, kelele,
matusi! Achaneni na kila uovu!
32 Muwe na moyo mwema na wenye kuhurumiana; kila mmoja na
amsamehe mwenzake kama naye Mungu alivyowasamehe ninyi kwa njia ya Kristo.
|