Chapter 6
1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu Kikristo maana hili ni
jambo jema.
2 "Waheshimu Baba na mama yako," hii ndiyo amri
ya kwanza ambayo imeongezewa ahadi, yaani,
3 "Upate fanaka na miaka mingi duniani."
4 Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni
katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo.
5 Enyi watumwa, watiini mabwana zenu hapa duniani kwa hofu
na tetemeko; fanyeni hivyo kwa unyofu wa moyo kana kwamba mnamtumikia Kristo.
6 Fanyeni hivyo si tu wakati wanapowatazama ili
mjipendekeze kwao, bali tumikieni kwa moyo kama atakavyo Mungu kwa sababu ninyi
ni watumishi wa Kristo.
7 Muwe radhi kutumikia kwa ajili ya Bwana na si kwa ajili
ya watu.
8 Kumbukeni kwamba kila mtu mwenye kutenda mema, awe mtumwa
au mtu huru, atapokea tuzo lake kutoka kwa Bwana.
9 Nanyi mnaotumikiwa, watendeeni vivyo hivyo watumwa wenu,
na acheni kutumia vitisho. Kumbukeni kwamba ninyi pia kama vile wao, mnaye
Bwana yuleyule mbinguni, kwake cheo cha mtu si kitu.
10 Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana
na kwa msaada wa nguvu yake kuu.
11 Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu
mbaya za Ibilisi.
12 Maana vita vyenu si vita kati yetu na binadamu, bali ni
vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na
wenye nguvu wanaomiliki ulimwengu huu wa giza.
13 Kwa sababu hiyo, vaeni silaha za Mungu ili siku ile
itakapofika muweze kuyapinga mashambulio ya adui; na mkisha pigana mpaka
mwisho, muwe bado thabiti.
14 Basi, simameni imara! Ukweli uwe kama ukanda kiunoni
mwenu, uadilifu uwe kama vazi la kujikinga kifuani,
15 na hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani iwe kama
viatu miguuni mwenu.
16 Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi
mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu.
17 Upokeeni wokovu kama kofia yenu ya chuma, na neno la
Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu.
18 Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila
wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote
wa Mungu.
19 Niombeeni nami pia ili niongeapo Mungu anijalie cha
kusema, niweze kuwajulisha watu fumbo la Habari Njema kwa uthabiti.
20 Mimi ni balozi kwa ajili ya Habari Njema hiyo ingawa
sasa niko kifungoni. Ombeni, basi, ili niweze kuwa hodari katika kuitangaza
kama inipasavyo.
21 Tukiko, ndugu yetu mpenzi na mtumishi mwaminifu wa
Bwana, atawapeni habari zangu zote mpate kujua ninachofanya.
22 Namtuma kwenu awapeni habari zetu mpate kuwa na moyo.
23 Ninawatakieni ninyi ndugu amani, upendo na imani kutoka
kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.
24 Nawatakia neema ya Mungu wote wanaompenda Bwana wetu
Yesu Kristo kwa mapendo yasiyo na mwisho.
|