Colossians
Chapter 1
1 Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na
ndugu Timotheo,
2 tunawaandikia ninyi watu wa Mungu huko Kolosai, ndugu
zetu waaminifu katika kuungana na Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka
kwa Mungu Baba yetu.
3 Daima tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
wakati tunapowaombea.
4 Maana tumesikia juu ya imani yenu katika Kristo Yesu na
juu ya upendo wenu kwa watu wote wa Mungu.
5 Wakati ujumbe ule wa kweli, yaani Habari Njema,
ilipowafikieni kwa mara ya kwanza, mlipata kusikia juu ya lile tumaini
linalopatikana kwake. Kwa sababu hiyo imani na upendo wenu vinategemea jambo
lile mnalotumainia ambalo mmewekewa salama mbinguni.
6 Habari Njema inazidi kuzaa matunda na kuenea ulimwenguni
kote kama vile ilivyofanya kwenu ninyi tangu siku ile mliposikia juu ya neema
ya Mungu na kuitambua ilivyo kweli.
7 Mlijifunza juu ya neema ya Mungu kutoka kwa Epafra,
mtumishi mwenzetu, ambaye ni mfanyakazi mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu.
8 Yeye alitupa habari za upendo wenu mliojaliwa na Roho.
9 Kwa sababu hiyo tumekuwa tukiwaombeeni daima tangu
tulipopata habari zenu. Tunamwomba Mungu awajazeni ujuzi kamili wa mapenzi
yake, awajazeni hekima yote na elimu iletwayo na Roho wake.
10 Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana na kutenda
daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya
matendo mema na mtazidi kukua katika kumjua Mungu.
11 Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili mweze
kustahimili kila kitu kwa uvumilivu.
12 Na kwa furaha, mshukuruni Baba aliyewawezesha ninyi kuwa
na sehemu yenu katika mambo yale Mungu aliyowawekea watu wake katika utawala wa
mwanga.
13 Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama
katika ufalme wa Mwanae mpenzi,
14 ambaye kwa njia yake tunakombolewa, yaani dhambi zetu
zinaondolewa.
15 Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana; ni mzaliwa wa
kwanza wa viumbe vyote.
16 Maana kwa njia yake vitu vyote viliumbwa duniani na
mbinguni, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana: wenye enzi, watawala, wakuu na
wenye mamlaka. Vyote viliumbwa kwa njia yake na kwa ajili yake.
17 Kristo alikuwako kabla ya vitu vyote; kwa kuungana naye,
vyote vyadumu mahali pake.
18 Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani kanisa; yeye ni
chanzo cha uhai wa huo mwili. Yeye ndiye mwanzo, mzaliwa wa kwanza
aliyefufuliwa kutoka wafu, ili awe na nafasi ya kwanza katika vitu vyote.
19 Maana Mungu alipenda utimilifu wote uwe ndani yake.
20 Kwa njia yake Mungu alivipatanisha naye vitu vyote naam,
viumbe vyote mbinguni na duniania; alileta amani kwa damu ya Kristo msalabani.
21 Hapo kwanza ninyi pia mlikuwa mbali na Mungu na mlikuwa
adui zake kwa sababu ya fikira zenu na matendo yenu maovu.
22 Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani,
Mungu amewapatanisha naye, kusudi awalete mbele yake mkiwa watakatifu, safi na
bila lawama.
23 Mnapaswa, lakini kuendelea kuwa imara na thabiti katika
imani hiyo, na msikubali kusukumwa mbali na tumaini lile mlilopata wakati
mlipoisikia Habari Njema. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Habari Njema
ambayo imekwisha hubiriwa kila kiumbe duniani.
24 Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa
mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika
mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa.
25 Nami nimefanywa kuwa mtumishi wa kanisa kufuatana na
mpango wake Mungu ambao alinikabidhi kwa faida yenu. Mpango wenyewe ni
kuutangaza kwa ukamilifu ujumbe wake,
26 ambao ni siri aliyowaficha binadamu wote tangu milele,
lakini sasa amewajulisha watu wake.
27 Mpango wa Mungu ni kuwajulisha watu wake siri hii kuu na
tukufu ambayo ni kwa ajili ya watu wote. Na, siri yenyewe ndiyo hii: Kristo
yuko ndani yenu, na jambo hilo lamaanisha kwamba ninyi mtaushiriki utukufu wa
Mungu.
28 Kwa sababu hiyo tunamhubiri Kristo kwa watu wote;
tunawaonya na kuwafundisha wote kwa hekima yote, ili tuweze kumleta kila mmoja
mbele ya Mungu akiwa amekomaa katika kuungana na Kristo.
29 Kwa madhumuni hayo mimi nafanya kazi na kujitahidi
nikiitumia nguvu kuu ya Kristo ifanyayo kazi ndani yangu.
|