Chapter 3
1 Basi, ikiwa mmefufuka pamoja na Kristo, panieni mambo ya
juu, kule Kristo aliko, ameketi upande wa kulia wa Mungu.
2 Muwe na hamu ya mambo ya huko juu, na siyo mambo ya hapa
duniani.
3 Maana ninyi mmekufa na uzima wenu umefichwa pamoja na
Kristo katika Mungu.
4 Uzima wenu halisi ni Kristo, na wakati atakapotokea ndipo
nanyi pia mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.
5 Basi, komesheni kabisa kila kitu kilicho ndani yenu
ambacho chahusika na mambo ya kidunia: uasherati, uchafu, shauku, tamaa mbaya
na uchu (ambao ni sawa na kuabudu sanamu).
6 Kwa sababu ya mambo hayo hasira ya Mungu huwajia wote
wanaomwasi.
7 Wakati mmoja ninyi pia mliishi kufuatana na mambo hayo,
mlipotawaliwa nayo.
8 Lakini sasa mnapaswa kuachana na mambo haya yote: hasira,
tamaa, uovu; kufuru au maneno yasiyofaa yasitoke kamwe vinywani mwenu.
9 Msiambiane uongo, kwani ninyi mmekwisha vua ule utu wa
kale pamoja na matendo yake yote,
10 mkavaa utu mpya. Huu unaendelea kurekebishwa na Mungu,
Muumba wake, kadiri ya mfano wake, ili mpate kumjua Mungu kwa ukamilifu.
11 Katika hali hii, hakuna tena tofauti kati ya Mgiriki na
Myahudi, aliyetahiriwa na asiyetahiriwa, msomi na asiye msomi, mtumwa na mtu
aliye huru. Kristo ni kila kitu, na yumo katika yote.
12 Ninyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua.
Kwa hiyo basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu.
13 Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo
lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe ninyi.
14 Zaidi ya hayo yote, zingatieni upendo kwani upendo
huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili.
15 Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa
ajili hiyo ninyi mmeitwa katika mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani!
16 Ujumbe wa Kristo ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake
wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni zaburi, nyimbo na
tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani.
17 Na, kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa
jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu Baba kwa njia yake.
18 Enyi akina mama, watiini waume zenu, kwani ndivyo
apendavyo Bwana.
19 Nanyi waume, wapendeni wake zenu, na msiwe wakali kwao.
20 Enyi watoto, watiini wazazi wenu daima maana hiyo
humpendeza Bwana.
21 Nanyi wazazi, msiwachukize watoto wenu, la sivyo
watakata tamaa.
22 Enyi watumwa, watiini wakuu wenu wa kidunia katika mambo
yote, na si tu wakati wanapowatazama kwa kuwa mnataka kujipendekeza kwao; ila
fanyeni hivyo kwa moyo wote, kwa sababu ya kumcha Bwana.
23 Kila mfanyalo, fanyeni kwa moyo wote, kwa sababu ya
Bwana na si kwa ajili ya mtu.
24 Kumbukeni kwamba atawapeni tuzo lile alilowawekea watu
wake. Mtumikieni Kristo Bwana!
25 Atendaye mabaya atalipwa kufuatana na ubaya wake; Mungu
hana ubaguzi.
|