Chapter 4
1 Nanyi wakuu, watendeeni watumwa wenu kwa uadilifu na
haki, mkikumbuka kwamba nanyi pia mnaye Bwana mbinguni.
2 Dumuni katika sala, na mnaposali muwe waangalifu,
mkimshukuru Mungu.
3 Vilevile, mtuombee sisi pia ili Mungu atupe fursa ya
kuuhubiri ujumbe wake kuhusu siri ya Kristo. Kwa ajili hiyo mimi niko sasa kifungoni.
4 Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa
namna itakayodhihirisha siri hiyo.
5 Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini,
mkitumia vizuri kila nafasi mliyo nayo.
6 Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na ya kuvutia,
na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja.
7 Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na
mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote.
8 Ndiyo maana namtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa
kuwaambieni habari zetu.
9 Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na
mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote
yanayofanyika hapa.
10 Aristarko, ambaye yuko kifungoni pamoja nami,
anawasalimuni; hali kadhalika Marko, binamu yake Barnaba, (mmekwisha pata
maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni).
11 Naye Yoshua aitwaye Yusto, anawasalimuni. Miongoni mwa
Wayahudi waliokwisha pokea imani, hawa tu peke yao, ndio wanaofanya kazi pamoja
nami kwa ajili ya Utawala wa Mungu; nao wamekuwa msaada mkubwa kwangu.
12 Epafra, mwananchi mwenzenu na mtumishi wa Kristo Yesu
anawasalimuni. Daima anawaombeeni ninyi kwa bidii ili mpate kusimama imara,
mkomae na kuwa thabiti kabisa katika mambo yote anayotaka Mungu.
13 Naweza kushuhudia kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa
ajili yenu na kwa ajili ya watu wa Laodikea na Hierapoli.
14 Luka, daktari wetu mpenzi, na Dema, wanawasalimuni.
15 Salamu zetu kwa ndugu zetu wa Laodikea; msalimuni dada
Nimfa pamoja na jumuiya yote ya waumini inayokutana nyumbani kwake.
16 Mkisha soma barua hii, hakikisheni kwamba inasomwa na
Wakristo wa Laodikea; na ninyi fanyeni mpango mpate kuisoma barua waliyoipata
kwao.
17 Mwambieni Arkipo aitekeleze vizuri ile huduma
aliyokabidhiwa na Bwana.
18 Naandika haya kwa mkono wangu mwenyewe: Salamu kutoka
kwangu, mimi Paulo. Kumbukeni kwamba niko kifungoni. Neema ya Mungu iwe nanyi.
|