1 Thessalonians
Chapter 1
1 Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi
jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba, na wa Bwana
Yesu Kristo.
2 Tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi nyote na
kuwakumbukeni daima katika sala zetu.
3 Maana, mbele ya Mungu Baba yetu, twakumbuka jinsi
mnavyoonyesha imani yenu kwa matendo, jinsi upendo wenu unavyowawezesha kufanya
kazi kwa bidii, na jinsi tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo lilivyo
thabiti.
4 Ndugu, twajua kwamba Mungu anawapenda na kwamba amewateua
muwe watu wake,
5 maana wakati tulipowahubirieni ile Habari Njema haikuwa
kwa maneno tu, bali pia kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu, tukiwa na hakika
kwamba ujumbe huo ulikuwa wa kweli. Mnajua jinsi tulivyoishi pamoja nanyi;
tuliishi kwa manufaa yenu.
6 Ninyi mlifuata mfano wetu, na kumwiga Bwana. Ingawa
mliteswa sana, mliupokea ujumbe huo kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu.
7 Kwa hiyo ninyi mmekuwa mfano mzuri kwa waumini wote wa
Makedonia na Akaya.
8 Maana, kutokana na bidii yenu ujumbe wa Bwana umesikika
si tu huko Makedonia na Akaya, bali imani yenu kwa Mungu imeenea popote. Tena
hatuhitaji kusema zaidi.
9 Watu hao wanazungumza juu ya ziara yetu kwenu: jinsi
mlivyotukaribisha, jinsi mlivyoziacha sanamu mkamgeukia Mungu aliye hai na wa
kweli,
10 na sasa mwamngojea Mwanae ashuke kutoka mbinguni, Yesu,
ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu, na ambaye anatuokoa katika ghadhabu ya
Mungu inayokuja.
|