Chapter 5
1 Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda mlimani,
akaketi. Wanafunzi wake wakamwendea,
2 naye akaanza kuwafundisha:
3 "Heri walio maskini rohoni, maana ufalme wa mbinguni
ni wao.
4 Heri walio na huzuni, maana watafarijiwa.
5 Heri walio wapole, maana watairithi nchi.
6 Heri wenye njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu, maana
watashibishwa.
7 Heri
walio na huruma, maana watahurumiwa.
8 Heri
wenye moyo safi, maana watamwona Mungu.
9 Heri
wenye kuleta amani, maana wataitwa watoto wa Mungu.
10 Heri
wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo Mungu, maana ufalme wa mbinguni ni
wao.
11
"Heri yenu ninyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila
aina ya uovu kwa ajili yangu.
12
Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo
walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu.
13
"Ninyi ni chumvi ya dunia! Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa
na nini? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu.
14
"Ninyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi
kufichika.
15 Wala
watu hawawashi taa na kuifunika kwa chungu, ila huiweka juu ya kinara ili
iwaangazie wote waliomo nyumbani.
16 Vivyo
hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu
mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni."
17
"Msidhani ya kuwa nimekuja kutangua Sheria ya Mose na mafundisho ya
manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha.
18 Kweli
nawaambieni, mpaka hapo mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata nukta moja au
sehemu ndogo kabisa ya Sheria itakayoondolewa, mpaka yote yametimia.
19 Basi,
yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine
wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika Ufalme wa mbiguni. Lakini yule
atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika Ufalme wa
mbinguni.
20 Ndiyo
maana nawaambieni, wema wenu usipozidi ule wa Mafarisayo na walimu wa Sheria,
hamtaingia kamwe katika Ufalme wa mbinguni.
21
"Mmekwisha sikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa: `Usiue! Atakayeua lazima
ahukumiwe.`
22 Lakini
mimi nawaambieni, yeyote anayemkasirikia ndugu yake, lazima ahukumiwe.
Anayemdharau ndugu yake atapelekwa mahakamani. Anayemwita ndugu yake: `Pumbavu`
atastahili kuingia katika moto wa Jehanamu.
23 Basi,
ukipeleka sadaka yako mbele ya madhabahu na hapo ukakumbuka kwamba ndugu yako
ana ugomvi nawe,
24 iache
sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako, ndipo
urudi ukatoe sadaka yako.
25
"Patana na mshtaki wako upesi mkiwa bado njiani, kwenda mahakamani. La
sivyo, mshtaki wako atakukabidhi kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa
askari, nawe utafungwa gerezani.
26 Kweli
nakwambia, hutatoka humo mpaka umemaliza kulipa senti ya mwisho.
27
"Mmesikia ya kuwa watu waliambiwa: `Usizini!`
28 Lakini
mimi nawaambieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye
moyoni mwake.
29 Basi,
kama jicho lako la kulia linakukosesha, ling`oe ukalitupe mbali. Afadhali zaidi
kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote kutupwa
katika moto wa Jehanamu.
30 Na kama
mkono wako wa kulia unakukosesha, ukate ukautupe mbali. Afadhali zaidi kupoteza
kiungo kimoja cha mwili, kuliko mwili wako wote uende katika moto wa Jehanamu.
31
"Ilikwisha semwa pia: `Anayemwacha mke wake, yampasa ampe hati ya talaka.`
32 Lakini
mimi nawaambieni, anayempa mkewe talaka, isipokuwa kwa sababu ya uzinzi,
anamfanya azini; na mtu akimwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini.
33
"Tena mmesikia kuwa watu wa kale waliambiwa: `Usivunje kiapo chako, bali
ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana.`
34 Lakini
mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha
Mungu;
35 wala
kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni
mji wa Mfalme mkuu.
36 Wala
usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe
au mweusi.
37
Ukisema, `Ndiyo`, basi iwe `Ndiyo`; ukisema `Siyo`, basi iwe kweli `Siyo`.
Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu.
38
"Mmesikia kwamba ilisemwa: `Jicho kwa jicho, jino kwa jino.`
39 Lakini
mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la
kulia, mgeuzie pia shavu la pili.
40 Mtu
akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwache achukue pia koti
lako.
41 Mtu
akikulazimisha kubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili.
42
Akuombaye mpe, na mtu akitaka kukukopa kitu usimnyime.
43
"Mmesikia kwamba ilisemwa: `Mpende jirani yako na kumchukia adui yako.`
44 Lakini
mimi nawaambieni, wapendeni adui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu ninyi
45 ili
mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua
lake watu wabaya na wema, na kuwanyeshea mvua watu wanyofu na waovu.
46 Je,
mtapata tuzo gani kwa kuwapenda tu wale wanaowapenda ninyi? Hakuna! Kwa maana
hata watoza ushuru hufanya hivyo!
47 Kama
mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mmefanya kitu kisicho cha kawaida? Hata watu
wasiomjua Mungu nao hufanya vivyo hivyo.
48 Basi,
muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.
|