Chapter 2
1 Ndugu, ninyi wenyewe mnafahamu kwamba ziara yetu kwenu
haikuwa bure.
2 Mnajua jinsi tulivyodhulumiwa na kutukanwa kule Filipi
kabla ya kufika kwenu Thesalonike. Ingawa kulikuwa na upinzani mwingi, Mungu
wetu alitujalia uhodari wa kuwahubirieni Habari Njema yake.
3 Jambo tunalosisitiza kwenu si jambo linalotegemea uongo
au nia mbaya; wala hatupendi kumdanganya mtu yeyote.
4 Sisi twanena daima kama atakavyo Mungu kwani yeye
alituona kwamba tunafaa, akatukabidhi hii Habari Njema. Si nia yetu kuwapendeza
watu hata kidogo, bali twataka kumpendeza Mungu ambaye anajua mioyo yetu mpaka
ndani.
5 Ninyi mnajua kwamba sisi hatukuja kwenu na maneno matamu
ya kubembeleza wala hatukutumia maneno ya kijanja ya kuficha ubinafsi fulani;
Mungu ni shahidi!
6 Hatukutafuta sifa kutoka kwa watu, wala kutoka kwenu,
wala kutoka kwa mtu yeyote,
7 ingawa sisi tukiwa mitume wa Kristo, tungeweza kudai
mambo fulani kwenu. Lakini sisi tulikuwa Wapole kati yenu kama alivyo mama kwa
watoto wake.
8 Tuliwapenda ninyi sana hata tukawa tayari kuwashirikisha si
tu Habari Njema ya Mungu, bali pia na maisha yetu. Ndivyo mlivyokuwa wapenzi
wetu!
9 Ndugu, mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi na kutaabika.
Tulipowaleteeni Habari Njema ya Mungu tulifanya kazi mchana na usiku kusudi
tusiwe mzigo kwa mtu yeyote miongoni mwenu.
10 Ninyi mnaweza kushuhudia, na Mungu pia ni shahidi, jinsi
mwenendo wetu kati yenu ninyi mnaoamini ulivyokuwa mzuri, mwadilifu na usio na
lawama.
11 Mnajua kwamba sisi tulimtendea kila mmoja wenu kama vile
baba anavyowatendea watoto wake mwenyewe.
12 Tuliwapeni moyo, tuliwafarijini na kuwahimiza ili mpate
kuishi maisha yampendezayo Mungu ambaye aliwaiteni mshiriki Utawala na utukufu
wake.
13 Tena tunayo sababu nyingine ya kumshukuru Mungu:
tulipowaleteeni ujumbe wa Mungu, ninyi mliusikia mkaupokea, si kama vile ujumbe
wa binadamu, bali kama ujumbe wa Mungu, na kweli ndivyo ulivyo. Maana Mungu
anafanya kazi ndani yenu ninyi mnaoamini.
14 Ndugu, ninyi mmepatwa na mambo yaleyale yaliyoyapata
makanisa ya Mungu kule Yudea, mambo yaliyowapata watu walio wake Kristo Yesu.
Ninyi mlidhulumiwa na wananchi wenzenu kama vile wao walivyodhulumiwa na wenzao
Wayahudi,
15 ambao walimuua Bwana Yesu na manabii, wakatutesa na sisi
pia. Watu hao wanamchukiza Mungu, tena ni adui za kila mtu!
16 Hata walijaribu kutuzuia kuwahubiria watu wa mataifa
mengine ujumbe utakaowaletea wokovu. Ndivyo walivyokamilisha orodha ya dhambi
zote walizotenda siku zote. Lakini sasa hasira ya Mungu imewaangukia.
17 Ndugu, kuachana kwetu nanyi kulikuwa kwa muda tu, tena
kuachana huko kulikuwa kwa mwili tu na si kwa roho. Kitambo kifupi baadaye,
tulishikwa na hamu kubwa ya kuwaoneni tena!
18 Kwa hiyo tuliamua kuwatembeleeni tena. Nami, Paulo,
nilijaribu kuja kwenu zaidi ya mara moja, lakini Shetani alituzuia.
19 Je, tutakaposimama mbele ya Bwana Yesu wakati
atakapokuja, fahari ya ushindi wetu itakuwa nini? Itakuwa ni ninyi wenyewe;
ninyi ndio tumaini letu na furaha yetu.
20 Naam, ninyi ni utukufu wetu na furaha yetu!
|