Chapter 2
1 Sasa yahusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na
kukusanywa kwetu pamoja tukae naye. Ndugu, tunawaombeni sana
2 msifadhaike upesi moyoni, na wala msitiwe wasiwasi kwa sababu
ya madai kwamba Siku ya Bwana imekwisha fika. Labda inadhaniwa kwamba jambo
hili limetokana na uaguzi fulani, mahubiri au barua inayosemekana kuwa imetoka
kwetu.
3 Msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa namna yoyote ile.
Maana Siku hiyo haitakuja mpaka kwanza ule Uasi Mkuu utokee na yule Mwovu
aonekane ambaye mwisho wake ni kuangamizwa kabisa.
4 Yeye atapinga kila kitu wanachokiona watu kuwa ni mungu,
au wanachokiabudu. Naam, hata ataingia na kuketi ndani ya Hekalu la Mungu
akijidai kuwa Mungu.
5 Je, hamkumbuki kwamba niliwaambieni haya yote wakati
nilipokuwa pamoja nanyi?
6 Lakini kuna kitu kinachomzuia sasa, nanyi mwakijua kitu
hicho. Basi, huyo Mwovu ataonekana wakati wake ufaao.
7 Hata hivyo, Mwovu huyo aliyefichika anafanya kazi sasa,
lakini hataonekana mpaka yule anayemzuia aondolewe.
8 Hapo ndipo Mwovu atakapotokea; lakini Bwana Yesu
anapokuja atamuua kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kwa mng`ao wa kuja
kwake.
9 Huyo Mwovu atakuja na nguvu za Shetani na kufanya kila
namna ya miujiza na maajabu ya uongo,
10 na kutumia udanganyifu wa kila namna kwa wale walio
katika mkumbo wa kupotea. Hao watapotea kwa sababu hawakuupokea na kuupenda ule
ukweli ili waokolewe.
11 Ndiyo maana Mungu amewaweka chini ya nguvu ya upotovu,
wauamini uongo.
12 Matokeo yake ni kwamba wote wasioamini ukweli, ila
wafurahia dhambi, watahukumiwa.
13 Tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi
ndugu, ninyi mnaopendwa na Bwana, kwa maana Mungu amewateua tangu mwanzo mpate
kuokolewa kwa nguvu ya Roho mfanywe watu wake watakatifu kwa imani yenu katika
ukweli.
14 Mungu aliwaitieni jambo hili kwa njia ya Habari Njema
tuliyowahubirieni; aliwaiteni mpate kupokea sehemu yenu katika utukufu wa Bwana
wetu Yesu Kristo.
15 Basi, ndugu, simameni imara na zingatieni yale
mafundisho tuliyowafundisheni kwa mahubiri yetu na barua zetu.
16 Tunamwomba Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba
yetu ambaye alitupenda, na kwa neema yake akatujalia faraja ya milele na
tumaini jema,
17 aifariji mioyo yenu na kuwaimarisheni ili mweze daima
kutenda na kusema yaliyo mema.
2 Thessalonians
|