1 Timothy
Chapter 1
1 Mimi
Paulo, mtume wa Yesu Kristo kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Yesu Kristo
tumaini letu,
2
nakuandikia Timotheo mwanangu halisi katika imani. Nakutakia neema, huruma na
amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu Bwana wetu.
3 Napenda
ukae huko Efeso, kama nilivyokuomba nilipokuwa ninakwenda Makedonia. Wako watu
fulani huko wanaofundisha mafundisho ya uongo. Wakomeshe watu hao.
4 Waambie
waachane na zile hadithi tupu na orodha ndefu za mababu, ambazo huleta tu
ubishi, wala haviwajengi watu katika mpango ujulikanao kwa imani.
5 Shabaha
ya amri hii ni kuhimiza mapendo yatokayo katika moyo safi, dhamiri njema, na
imani ya kweli.
6 Watu
wengine wamepotoka na kugeukia majadiliano yasiyo na maana.
7
Wanapenda kuwa walimu wa Sheria, lakini hawaelewi maneno yao wenyewe au mambo
wanayosisitiza.
8 Twajua
kwamba Sheria ni njema, kama ikitumiwa ipasavyo.
9 Lakini
tunapaswa kukumbuka kwamba sheria haziwekwi kwa ajili ya watu wema, bali kwa
ajili ya wahalifu na wasiotii, wasiomcha Mungu na wenye dhambi, watu wasio na
dini na wa kidunia. Watu wanaowaua baba na mama zao, au wauaji wowote wale;
10 sheria
imewekwa kwa ajili ya waasherati, wafiraji, wanaowaiba watu, waongo, na
wanaoapa uongo au wanaofanya chochote ambacho ni kinyume cha mafundisho ya
kweli.
11 Mafundisho
hayo hupatikana katika Habari Njema ambayo mimi nimekabidhiwa niihubiri, Habari
Njema ya Mungu mtukufu na mwenye heri.
12
Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu.
Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie,
13 ingawa
pale awali mimi nilimtukana na kumtesa na kumdhulumu. Lakini Mungu alinionea
huruma, kwa sababu sikuwa na imani bado, na hivyo sikujua nilichokuwa
ninafanya.
14 Lakini
Bwana wetu alinijalia neema yake kwa wingi, akanipa imani na upendo katika
kuungana na Kristo Yesu.
15 Usemi
huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja
ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Nami ni mkosefu zaidi kuliko hao wote,
16 lakini
Mungu alinionea huruma, ili Kristo aonyeshe uvumilivu wake wote kwangu mimi,
kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uzima wa milele.
17 Kwake
yeye aliye Mfalme wa milele na asiyekufa, yeye aliye Mungu pekee - kwake viwe
heshima na utukufu milele na milele! Amina.
18
Mwanangu Timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii
yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika kupigana
vita vizuri,
19 na
ushike imani yako na dhamiri njema. Watu wengine hawakusikiliza dhamiri zao na
hivyo wakaiharibu imani yao.
20
Miongoni mwao ni Humenayo na Aleksanda ambao nimewakabidhi kwa Shetani, ili
wafundishwe wasimtukane Mungu.
|