Chapter 2
1 Kwanza
kabisa, basi naomba dua, sala, maombi na sala za shukrani zitolewe kwa Mungu
kwa ajili ya watu wote,
2 kwa
ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na
amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema.
3 Jambo
hili ni jema na lampendeza Mungu Mwokozi wetu,
4 ambaye
anataka watu wote waokolewe na wapate kuujua ukweli.
5 Maana
yuko Mungu mmoja, na pia yuko mmoja anayewapatanisha watu na Mungu, binadamu
Kristo Yesu,
6 ambaye
alijitoa mwenyewe kuwakomboa watu wote. Huo ulikuwa uthibitisho, wakati ufaao
ulipowadia.
7 Kwa sababu
hiyo mimi nilitumwa niwe mtume na mwalimu wa watu wa mataifa, niutangaze ujumbe
wa imani na ukweli. Nasema ukweli; sisemi uongo!
8 Basi,
popote mnapokutana kufanya ibada nataka wanaume wasali, watu waliojitolea kweli
na ambao wanaweza kuinua mikono yao wakisali bila hasira wala ubishi.
9 Hali
kadhalika, nawataka wanawake wawe wanyofu na wenye busara kuhusu mavazi yao;
wavae sawasawa na si kwa urembo wa mitindo ya kusuka nywele, kujipamba kwa
dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa,
10 bali
kwa matendo mema kama iwapasavyo wanawake wamchao Mungu.
11
Wanawake wanapaswa kukaa kimya na kuwa wanyenyekevu wakati wa kujifunza.
12 Mimi
simruhusu mwanamke amfundishe au amtawale mwanamume; anapaswa kukaa kimya.
13 Maana
Adamu aliumbwa kwanza, halafu Hawa.
14 Na wala
si Adamu aliyedanganywa; bali mwanamke ndiye aliyedanganywa, akaivunja sheria
ya Mungu.
15 Hata hivyo,
mwanamke ataokolewa kwa kupata watoto, kama akidumu katika imani, upendo,
utakatifu na unyofu.
|