Chapter 3
1 Msemo
huu ni wa kweli: mtu akitaka kuwa kiongozi katika kanisa, huyo anatamani kazi
nzuri.
2 Basi,
kiongozi wa kanisa anapaswa awe mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke mmoja
tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu; ni lazima awe mkarimu na anayeweza
kufundisha;
3 asiwe
mlevi au mtu wa matata, bali awe mpole, apendaye amani; asiwe mtu wa kupenda
fedha;
4 anapaswa
awe mtu awezaye kuongoza vema nyumba yake, na kuwafanya watoto wake wawe watii
kwa heshima yote.
5 Maana
kama mtu hawezi kuongoza vema nyumba yake, atawezaje kulitunza kanisa la Mungu?
6 Mtu
ambaye hajakomaa bado katika imani asifanywe kuwa kiongozi katika kanisa, asije
akajaa majivuno na kuhukumiwa kama vile Ibilisi alivyohukumiwa.
7 Anapaswa
awe mwenye sifa njema kati ya watu walio nje ya kanisa, ili asije akalaumiwa na
kuanguka katika mtego wa Ibilisi.
8
Wasaidizi katika kanisa wanapaswa pia kuwa watu wenye tabia njema na wanyofu;
wasiwe wanywaji mno wa divai au wenye tamaa ya fedha;
9
wanapaswa kuzingatia kwa dhamiri njema ukweli wa ndani wa imani.
10 Ni
lazima kwanza wathibitishwe, na wakionekana kuwa wanafaa, basi, watoe huduma
yao.
11 Wake
zao wanapaswa pia kuwa na tabia njema, wasiowasengenya watu, wenye kiasi na
waaminifu katika mambo yote.
12
Msaidizi katika kanisa lazima awe na mke moja tu, na awezaye kuongoza vema
watoto wake na nyumba yake.
13 Maana
wasaidizi wanaofanya kazi yao vizuri hujipatia msimamo mzuri, na wanaweza
kusema bila hofu juu ya imani yao katika Kristo Yesu.
14
Ninakuandikia barua hii nikiwa na matumaini ya kuja kwako hivi karibuni.
15 Lakini
kama nikicheleweshwa, basi, barua hii itakufahamisha mwenendo tunaopaswa kuwa
nao katika nyumba ya Mungu, ambayo ni kanisa la Mungu aliye hai, na ambalo ni
nguzo na msingi wa ukweli.
16 Hakuna
mashaka yoyote juu ya ukuu wa siri ya dini yetu: Alionekana katika umbo la
kibinadamu alithibitishwa na Roho kuwa ni mwadilifu, akaonekana na malaika.
Alihubiriwa kati ya mataifa, aliaminiwa popote ulimwenguni, akachukuliwa juu
mbinguni katika utukufu.
|