Chapter 6
1 Watumwa
wote wanapaswa kuwaheshimu wakuu wao ili kusiwe na sababu ya watu kulitukana
jina la Mungu na mafundisho yetu.
2 Watumwa
ambao wakuu wao ni Wakristo wasiwadharau kwani ni ndugu zao. Badala yake,
wanapaswa kuwatumikia hata vizuri zaidi, maana hao wanaopata faida kutokana na
kazi yao ni waumini ambao wanawapenda. Unapaswa kufundisha na kuhubiri mambo
haya.
3 Mtu
yeyote anayefundisha kinyume cha mambo haya, na ambaye hakubaliani na maneno ya
kweli ya Bwana wetu Yesu Kristo na mafundisho ya dini,
4 huyo
amejaa majivuno na wala hajui chochote. Ni mtu wa kupenda ubishi na magombano
juu ya maneno matupu, na hiyo husababisha wivu, ugomvi, matusi, shuku mbaya,
5 na ubishi
usio na kikomo kutoka kwa watu ambao akili zao zimeharibika, na ambao hawana
tena ukweli. Wanadhani dini ni njia ya kujipatia utajiri.
6 Kweli
dini humfanya mtu awe tajiri sana, ikiwa anatosheka na vitu alivyo navyo.
7 Maana
hatukuleta kitu chochote hapa duniani, wala hatutachukua chochote.
8 Kwa hiyo
basi, kama tunacho chakula na mavazi, tunapaswa kuridhika navyo.
9 Lakini
wale wanaotaka kutajirika huanguka katika majaribu, na kunaswa katika mtego wa
tamaa nyingi mbaya za kipumbavu, ambazo huwavuta mpaka kwenye uharibifu na
maangamizi.
10 Kwa maana kupenda sana fedha ni chanzo cha uovu wote.
Watu wengine wametamani sana kupata fedha hata wakatangatanga mbali na imani,
na wameivunja mioyo yao kwa huzuni nyingi.
11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, jiepushe na mambo hayo.
Zingatia uadilifu, uchaji wa Mungu, imani, mapendo, subira na unyenyekevu.
12 Piga mbio kadiri uwezavyo katika shindano la mbio za
imani, ukajipatie tuzo la uzima wa milele, uliloitiwa wakati ulipokiri imani
yako mbele ya mashahidi wengi.
13 Mbele ya Mungu anayevipa vitu vyote uhai, na mbele ya
Yesu Kristo aliyetoa ushahidi na kukiri ukweli mbele ya Pontio Pilato,
14 nakuamuru ushike maagizo yako na kuyatii kwa uaminifu
mpaka Siku ile atakapotokea Bwana wetu Yesu Kristo.
15 Kutokea kwake kutafanyika wakati ufaao uliopangwa na
Mungu mwenye heri na aliye Mtawala pekee, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa
mabwana.
16 Yeye peke yake anaishi milele, katika mwanga usioweza
kukaribiwa na mtu. Hakuna mtu aliyepata kumwona au awezaye kumwona. Kwake iwe
heshima na uwezo wa milele! Amina.
17 Waamuru watu walio matajiri katika mambo ya maisha ya
sasa, wasijivune, wasiweke tumaini lao katika mali isiyoweza kutegemewa; bali
wamtegemee Mungu, ambaye kwa ukarimu hutupatia vitu vyote tuvifurahie.
18 Waamuru watende mema, wawe matajiri katika matendo mema,
na wawe wakarimu na walio tayari kuwashirikisha wengine mali zao.
19 Kwa namna hiyo watajiwekea hazina ambayo itakuwa kwao
msingi imara kwa wakati ujao. Hapo wataweza kujipatia uzima ambao ni uzima wa
kweli.
20 Timotheo, tunza salama yote yale uliyokabidhiwa.
Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ubishi wa kipumbavu juu ya kile
wanachokiita watu wengine: "Elimu".
21 Maana wengine wamejidai kuwa na hiyo elimu, na matokeo
yake wamepoteza imani. Nawatakieni nyote neema!
|