2 Timothy
Chapter 1
1 Mimi Paulo, ambaye Mungu alitaka niwe mtume wa Kristo
Yesu ili niutangaze ule uzima tulioahidiwa katika kuungana na Kristo Yesu,
2 nakuandikia wewe mwanangu mpenzi Timotheo. Nakutakia
neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.
3 Ninamshukuru Mungu ambaye ninamtumikia kwa dhamiri safi
kama walivyofanya wazee wangu; namshukuru kila ninapokukumbuka daima katika
sala zangu.
4 Nakumbuka machozi yako na ninatamani usiku na mchana
kukuona, ili nijazwe furaha.
5 Naikumbuka imani yako ya kweli, imani aliyokuwa nayo
nyanya yako Loisi, na pia mama yako Eunike. Nina hakika kwamba wewe pia unayo.
6 Ndio maana nakukumbusha ukiweke motomoto kile kipaji
ulichopewa na Mungu wakati nilipokuwekea mikono yangu.
7 Kwa maana Mungu hakutupa Roho wa kutufanya tuwe waoga, bali
alitupa Roho wa kutujalia nguvu, upendo na nidhamu.
8 Basi, usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usione
haya kwa sababu yangu mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Lakini shiriki katika
mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unazopewa na Mungu.
9 Yeye alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si
kwa sababu ya matendo yetu wenyewe bali kwa sababu ya kusudi lake na neema
yake. Alitujalia neema hiyo katika Kristo Yesu kabla mwanzo wa nyakati;
10 lakini sasa imefunuliwa kwetu kwa kuja kwake Mwokozi
wetu Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema
akadhihirisha uzima usio kufa.
11 Mungu amenichagua mimi niwe mtume na mwalimu kwa ajili
ya kuhubiri Habari Njema,
12 nami nateseka mambo haya kwa sababu hiyo. Lakini niko
bado timamu kabisa kwani namjua yule niliyemwamini, tena nina hakika kwamba
yeye aweza kukilinda salama kile alichonikabidhi, mpaka Siku ile.
13 Shika kwa makini mafundisho yale ya kweli
niliyokufundisha, na kubaki katika hiyo imani na huo upendo wetu katika
kuungana na Kristo Yesu.
14 Jambo lile bora ulilokabidhiwa lilinde kwa nguvu ya Roho
Mtakatifu anayeishi ndani yetu.
15 Kama unavyojua, watu wote mkoani Asia wameniacha,
miongoni mwao wakiwa Fugelo na Hermogene.
16 Bwana aihurumie jamaa ya Onesiforo, kwa sababu
aliniburudisha rohoni mara nyingi, wala hakuona haya kwa kuwa nilikuwa kifungoni,
17 ila mara tu alipofika Roma, alianza kunitafuta kwa bidii
mpaka akanipata.
18 Bwana amjalie huruma katika Siku ile! Nawe wajua vizuri
mengi aliyonifanyia huko Efeso.
|