Chapter 2
1 Basi, wewe mwanangu, uwe na nguvu katika neema tunayopata
katika kuungana na Kristo Yesu.
2 Chukua yale mafundisho uliyonisikia nikitangaza mbele ya
mashahidi wengi, uyakabidhi kwa watu wanaoaminika, ambao wataweza kuwafundisha
wengine pia.
3 Shiriki katika mateso kama askari mwaminifu wa Kristo
yesu.
4 Mwanajeshi vitani hujiepusha na shughuli za maisha ya
kawaida ili aweze kumpendeza mkuu wa jeshi.
5 Mwanariadha yeyote hawezi kushinda na kupata zawadi ya
ushindi kama asipozitii sheria za michezo.
6 Mkulima ambaye amefanya kazi ngumu anastahili kupata
sehemu ya kwanza ya mavuno.
7 Fikiria hayo ninayosema, kwani Bwana atakuwezesha
uyaelewe yote.
8 Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka wafu, aliyekuwa
wa ukoo wa Daudi, kama isemavyo Habari Njema ninayoihubiri.
9 Kwa sababu ya kuihubiri Habari Njema mimi nateseka na
nimefungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu haliwezi kufungwa
minyororo,
10 na hivyo navumilia kila kitu kwa ajili ya wateule wa
Mungu, ili wao pia wapate ukombozi upatikanao kwa njia ya Yesu Kristo, na ambao
huleta utukufu wa milele.
11 Usemi huu ni wa kweli: "Ikiwa tulikufa pamoja naye,
tutaishi pia pamoja naye.
12 Tukiendelea kuvumilia, tutatawala pia pamoja naye.
Tukimkana, naye pia atatukana.
13 Tukikosa kuwa waaminifu, yeye hubaki mwaminifu daima,
maana yeye hawezi kujikana mwenyewe."
14 Basi, wakumbushe watu wako mambo haya, na kuwaonya mbele
ya Mungu waache ubishi juu ya maneno. Ubishi huo haufai, ila huleta tu
uharibifu mkuu kwa wale wanaousikia.
15 Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama
mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake, na ambaye hufundisha sawa ule
ujumbe wa kweli.
16 Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ya kipumbavu;
kwani hayo huzidi kuwatenga watu mbali na Mungu.
17 Mafundisho ya aina hiyo ni kama donda linalokula mwili.
Miongoni mwa hao waliofundisha hayo ni Humenayo na Fileto.
18 Hawa wamepotoka kabisa mbali na ukweli, na wanatia imani
ya watu wengine katika wasiwasi kwa kusema ati ufufuo wetu umekwisha fanyika.
19 Lakini msingi thabiti uliowekwa na Mungu uko imara, na
juu yake yameandikwa maneno haya: "Bwana anawafahamu wale walio
wake," na "Kila asemaye yeye ni wa Bwana, ni lazima aachane na
uovu."
20 Katika nyumba kubwa kuna mabakuli na vyombo vya kila
namna: vingine ni vya fedha na dhahabu, vingine vya mbao na udongo, vingine ni
vya matumizi ya pekee na vingine kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
21 Basi, kama mtu atajitakasa kwa kujitenga mbali na mambo
hayo yote maovu, atakuwa chombo cha matumizi ya pekee, kwa sababu amewekwa
wakfu, anamfaa Bwana wake na yupo tayari kwa kila kazi njema.
22 Jiepushe na tamaa za ujana, fuata uadilifu, imani,
upendo, amani, pamoja na watu wote ambao wanamwomba Bwana kwa moyo safi.
23 Epuka ubishi wa kijinga na kipumbavu; wajua kwamba hayo
huleta magomvi.
24 Mtumishi wa Bwana asigombane. Anapaswa kuwa mpole kwa
watu wote, mwalimu mwema na mvumilivu,
25 ambaye ni mpole anapowaonya wapinzani wake, kwani huenda
Mungu akawajalia nafasi ya kutubu, wakapata kuujua ukweli.
26 Hapo fahamu zao zitawarudia tena, wakaponyoka katika
mtego wa Ibilisi aliyewanasa na kuwafanya wayatii matakwa yake.
|