Chapter 3
1 Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati
za taabu.
2 watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye
majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na
shukrani na waovu;
3 watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma,
wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema;
4 watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda
anasa kuliko kumpenda Mungu.
5 Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini
wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo.
6 Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka
wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za
kila aina;
7 wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi
kuufikia ujuzi wa huo ukweli.
8 Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre
walivyompinga Mose.
9 Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana
wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre.
10 Wewe lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo
wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo
wangu, subira yangu,
11 udhalimu
na mateso yangu. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra.
Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote.
12 Kila
mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu
lazima adhulumiwe.
13 Watu
waovu na wadanyanyifu watazidi kuwa waovu zaidi na zaidi kwa kuwadanganya
wengine na kudanganyika wao wenyewe.
14 Lakini
wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa, ukaukubali kabisa. Unawajua wale
waliokuwa walimu wako.
15
Unakumbuka kwamba tangu utoto wako umeyajua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza
kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu.
16
Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika
kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi
maisha adili,
17 ili mtu
anayemtumikia Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila tendo jema.
|