Chapter 2
1 Lakini
wewe unapaswa kuhubiri mafundisho safi.
2 Waambie
wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa
kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu.
3 Hali
kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe
wachongezi, au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema,
4 ili
wawazoeze kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto,
5 wawe na
kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili
ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa.
6
Kadhalika, wahimize vijana wawe na kiasi.
7 Katika
mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe
na uzito katika mafundisho yako.
8 Maneno
yako yasiwe na hitilafu yoyote ili adui zako waaibike wasipopata chochote
kibaya cha kusema juu yetu.
9 Watumwa
wanapaswa kuwatii wakuu wao na kuwapendeza katika mambo yote. Wasibishane nao,
10 au
kuiba vitu vyao. Badala yake wanapaswa kuonyesha kwamba wao ni wema na
waaminifu daima, ili, kwa matendo yao yote, wayapatie sifa njema mafundisho juu
ya Mungu, Mwokozi wetu.
11 Maana
neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote.
12 Neema
hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi
maisha adili na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa,
13 tukiwa
tunangojea siku ile ya heri tunayoitumainia, wakati utakapotokea utukufu wa
Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
14 Yeye
alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na
kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda
mema.
15 Basi,
fundisha mambo hayo na tumia mamlaka yako yote ukiwahimiza na kuwaonya
wasikilizaji wako. Mtu yeyote na asikudharau.
|