Chapter 3
1
Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa
kila namna kutenda mambo yote mema.
2 Waambie
wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikizano, wawe daima wapole
kwa kila mtu.
3 Maana,
wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa
tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia
nasi tukawachukia.
4 Lakini
wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu, ulipofunuliwa,
5
alituokoa. alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali
alituokoa kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia
tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji.
6 Mungu
alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu,
7 ili kwa
neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uzima wa milele
tunaoutumainia.
8 Jambo
hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini
Mungu, wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, ambayo ni mambo
mazuri na ya manufaa kwa watu.
9 Lakini
jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya Sheria. Mambo hayo
hayana faida yoyote na ni ya bure tu.
10 Mtu
anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye.
11 Wajua
kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba
amekosea.
12 Baada
ya kumtuma kwako Artema au Tukiko, fanya bidii kuja Nikopoli unione, maana
nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi.
13
Jitahidi kumsaidia mwana sheria Zena na Apolo ili waweze kuanza ziara zao na
uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji.
14 Ni
lazima watu wetu wajifunze kuutumia wakati wao katika kutenda mema ili wasaidie
katika mahitaji ya kweli, na maisha yao yawe ya kufaa.
15 Watu wote
walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani. Nawatakieni nyote neema ya Mungu.
|