Chapter 2
1 Kwa
sababu hiyo tunapaswa kuzingatia kwa makini zaidi yote tuliyosikia, ili tusije
tukapotoshwa.
2 Ujumbe
ule waliopewa wazee wetu na malaika ulionyeshwa kuwa kweli, hata mtu yeyote
ambaye hakuufuata au hakuutii aliadhibiwa kama alivyostahili.
3 Basi,
sisi tutaokokaje kama hatuujali wokovu mkuu kama huu? Kwanza Bwana mwenyewe
aliutangaza wokovu huu, na wale waliomsikia walituthibitishia kwamba ni kweli.
4 Mungu
pia aliongeza hapo ushahidi wake kwa kufanya kila namna ya miujiza na maajabu,
na kwa kuwagawia watu vipaji vya Roho Mtakatifu kadiri ya mapenzi yake.
5 Mungu
hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea
habari zake.
6 Tena
yasemwa mahali fulani katika Maandiko: "Mtu ni nini ee Mungu, hata
umfikirie; mwanaadamu ni nini hata umjali?
7
Ulimfanya kwa kitambo kidogo kuwa chini zaidi kuliko malaika; ukamvika taji ya utukufu
na heshima,
8 ukaweka
kila kitu chini ya miguu yake, avitawale." Yasemwa kwamba Mungu alimweka
mtu kuwa mtawala wa vitu vyote yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo,
hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa.
9 Lakini
twamwona Yesu ambaye alifanywa kwa kitambo kidogo kuwa chini zaidi kuliko
malaika, ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote. Sasa tunamwona
ametawazwa kwa utukufu na heshima kwa sababu ya kifo alichoteseka.
10 Ilikuwa
haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu
kuwa mkamilifu kabisa kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki
utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu.
11 Yeye
anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba
mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao ndugu zake;
12 kama
asemavyo: "Ee Mungu, nitawatangazia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu
katika kusanyiko lao."
13 Tena
asema: "Nitamwekea Mungu tumaini langu." Na tena: "Mimi niko hapa pamoja na watoto
alionipa Mungu."
14 Basi,
kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe
akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao. Alifanya hivyo ili kwa njia ya kifo
chake amwangamize Ibilisi, ambaye ana mamlaka juu ya kifo,
15 na
hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu yao ya
kifo.
16 Maana
ni wazi kwamba yeye hakuja kwa ajili ya kuwasaidia malaika, bali kama yasemavyo
Maandiko; "Anawasaidia wazawa wa Abrahamu."
17 Ndiyo
maana ilimbidi awe kama ndugu zake kwa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao
aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu
ziondolewe.
18 Na,
anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa.
|