Chapter 4
1 Mungu
alituahidia kwamba tutaweza kupata pumziko hilo alilosema. Basi, na tuogope ili
yeyote kati yenu asije akashindwa kupata pumziko hilo.
2 Maana
Habari Njema imehubiriwa kwetu kama vile ilivyohubiriwa kwa hao watu wa kale.
Lakini ujumbe huo haukuwafaa chochote, maana waliusikia lakini hawakuupokea kwa
imani.
3 Basi, sisi tunaoamini tunapata pumziko hilo aliloahidi
Mungu. Kama alivyosema: "Nilikasirika, nikaapa: `Hawataingia huko ambako
ningewapa pumziko."` Mungu alisema hayo ingawa kazi yake ilikuwa imekwisha
malizika tangu alipoumba ulimwengu.
4 Maana Maandiko yasema mahali fulani kuhusu siku ya saba:
"Mungu alipumzika siku ya saba, akaacha kazi zake zote."
5 Tena jambo hili lasemwa pia: "Hawataingia huko
ambako ningewapa pumziko."
6 Wale waliotangulia kuhubiriwa Habari Njema hawakupata
pumziko hilo kwa sababu hawakuamini. Wapo, basi, wengine ambao wangejaliwa
kulipata.
7 Jambo hili ni wazi, kwani Mungu aliweka siku nyingine
ambayo inaitwa "Leo". Miaka mingi baadaye Mungu alisema juu ya hiyo
siku kwa maneno ya Daudi katika Maandiko yaliyokwisha tajwa: "Kama
mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu."
8 Kama Yoshua angaliwapa watu hao hilo pumziko, Mungu
hangalisema baadaye juu ya siku nyingine.
9 Kwa hiyo, basi, bado lipo pumziko kwa watu wa Mungu kama
kule kupumzika kwake Mungu siku ya saba.
10 Maana, kila anayepata pumziko aliloahidi Mungu
atapumzika baada ya kazi yake kama vile pia Mungu alivyopumzika baada ya yake.
11 Basi, tujitahidi kupata pumziko hilo, ili asiwepo yeyote
miongoni mwenu atakayeshindwa, kama walivyofanya wao kwa sababu ya ukosefu wao
wa imani.
12 Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali zaidi kuliko
upanga wenye makali kuwili. Hukata kabisa mpaka mahali ambapo moyo na roho
hukutana, mpaka pale vikutanapo viungo vya mwili na mafuta. Neno hilo huchambua nia na fikira za mioyo ya
watu.
13 Hakuna
kiumbe chochote kilichofichika mbele ya Mungu; kila kitu kimefunuliwa wazi
mbele ya macho yake. Kwake, sisi sote tutapaswa kutoa hoja ya matendo yetu.
14 Basi,
tunapaswa kuzingatia kwa uthabiti imani tunayoiungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu
aliyeingia mpaka kwa Mungu mwenyewe - Yesu, Mwana wa Mungu.
15 Huyu
Kuhani Mkuu wetu si mmoja ambaye hawezi kutuunga mkono katika unyonge wetu, ila
ni Kuhani Mkuu ambaye alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda
dhambi.
16 Basi,
na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu, palipo na neema, ili
tukajipatie huruma na neema ya kutusaidia wakati wa lazima.
|