Chapter 5
1 Kila
kuhani mkuu huchaguliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya kumtumikia Mungu
kwa niaba yao, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi zao.
2 Maadamu
yeye mwenyewe yu dhaifu anaweza kuwaonea huruma wale wasiojua kitu na
wanaofanya makosa.
3 Na kwa
vile yeye mwenyewe ni dhaifu, anapaswa kutolea dhabihu si tu kwa ajili ya watu,
bali pia kwa ajili ya dhambi zake.
4 Hakuna
mtu awezaye kujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja
huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni.
5 Hali kadhalika
naye Kristo hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu
alimwambia: "Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa baba yako."
6 Alisema
pia mahali pengine: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani
wa Melkisedeki."
7 Yesu
alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba
Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye alisikilizwa kwa
sababu ya kumcha Mungu.
8 Lakini,
ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kutii kwa njia ya mateso.
9 Na
alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wale wote
wanaomtii,
10 naye
Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa
Melkisedeki.
11 Tunayo
Mengi ya kusema juu ya jambo hili, lakini ni vigumu kuwaelezeni, kwa sababu
ninyi si wepesi wa kuelewa.
12 Sasa
mngalipaswa kuwa tayari walimu, lakini mnahitaji bado mtu wa kuwafundisheni mafundisho
ya mwanzo ya ujumbe wa Mungu. Badala ya kula chakula kigumu, mnapaswa bado
kunywa maziwa.
13 Kila
anayepaswa kunywa maziwa huyo ni mtoto bado, hajui uadilifu ni nini.
14 Lakini
chakula kigumu ni kwa ajili ya watu waliokomaa, ambao wanaweza kubainisha mema
na mabaya.
|