Chapter 7
1 Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu, na kuhani wa Mungu
Mkuu. Abrahamu alipokuwa anarudi kutoka vitani ambako aliwaua wafalme,
Melkisedeki alikutana naye akambariki,
2 naye Abrahamu akampa sehemu ya kumi ya vitu vyote
alivyokuwa navyo. (Maana ya kwanza ya jina hili Melkisedeki ni "Mfalme wa
Uadilifu"; na, kwa vile yeye alikuwa mfalme wa Salemu, jina lake pia lina
maana ya "Mfalme wa Amani.")
3 Baba yake na mama yake hawatajwi, wala ukoo wake hautajwi;
haisemwi alizaliwa lini au alikufa lini. Anafanana na Mwana wa Mungu, na anaendelea kuwa kuhani daima.
4 Basi,
mwaona jinsi mtu huyu alivyokuwa maarufu. Baba Abrahamu alimpa sehemu moja ya
kumi ya vitu vyote alivyoteka vitani.
5 Tunajua
vilevile kwamba kufuatana na Sheria, wana wa Lawi ambao ni makuhani, wanayo
haki ya kuchukua sehemu ya kumi kutoka kwa watu, yaani ndugu zao, ingawaje nao
ni watoto wa Abrahamu.
6 Lakini
huyo Melkisedeki hakuwa wa ukoo wa Lawi, hata hivyo alipokea sehemu ya kumi
kutoka kwa Abrahamu; tena akambariki yeye ambaye alikuwa amepewa ahadi ya
Mungu.
7 Hakuna
mashaka hata kidogo kwamba anayebariki ni mkuu zaidi kuliko yule anayebarikiwa.
8 Tena,
hao makuhani wanaopokea sehemu ya kumi, ni watu ambao hufa; lakini hapa
anayepokea sehemu ya kumi, yaani Melkisedeki, anasemekana kwamba hafi.
9 Twaweza,
basi, kusema kwamba Abrahamu alipotoa sehemu moja ya kumi, Lawi (ambaye watoto
wake hupokea sehemu moja ya kumi) alitoa sehemu moja ya kumi pia.
10 Maana
Lawi hakuwa amezaliwa bado, bali ni kama alikuwa katika mwili wa baba yake,
Abrahamu, wakati Melkisedeki alipokutana naye.
11
Kutokana na ukuhani wa Walawi, watu wa Israeli walipewa Sheria. Sasa, kama
huduma ya Walawi ingalikuwa kamilifu hapangekuwa tena na haja ya kutokea
ukuhani mwingine tofauti, ukuhani ambao umefuata utaratibu wa ukuhani wa
Melkisedeki, na si ule wa Aroni.
12 Maana
ukuhani ukibadilika ni lazima Sheria nayo ibadilike.
13 Naye
Bwana wetu ambaye mambo hayo yote yanasemwa juu yake, alikuwa wa kabila
lingine, na wala hakuna hata mmoja wa kabila lake aliyepata kutumikia
madhabahuni akiwa kuhani.
14
Inafahamika wazi kwamba yeye alizaliwa katika kabila la Yuda ambalo Mose
hakulitaja alipokuwa anasema juu ya makuhani.
15 Tena
jambo hili ni dhahiri zaidi: kuhani mwingine anayefanana na Melkisedeki
amekwisha tokea.
16 Yeye
hakufanywa kuwa kuhani kwa sheria na maagizo ya kibinadamu, bali kwa nguvu ya
uhai ambao hauna mwisho.
17 Maana
Maandiko yasema: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani
wa Melkisedeki."
18 Basi,
ile amri ya zamani ilifutwa kwa sababu ilikuwa hafifu na isiyofaa kitu.
19 Maana
Sheria ya Mose haikuweza kukamilisha jambo lolote. Lakini sasa, mahali pake
pamewekwa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo tunaweza kumkaribia Mungu.
20 Zaidi
ya hayo hapa pana kiapo cha Mungu. Wakati wale wengine walipofanywa makuhani
hapakuwako kiapo.
21 Lakini
Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia: "Bwana ameapa,
wala hataigeuza nia yake: `Wewe ni kuhani milele."`
22 Basi,
kutokana na tofauti hii, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.
23 Kuna
tofauti nyingine pia: hao makuhani wengine walikuwa wengi kwa sababu walikufa
na hawakuweza kuendelea na kazi yao.
24 Lakini
Yesu si kama wao, yeye anaishi milele; ukuhani wake hauondoki kwake.
25 Hivyo,
yeye anaweza daima kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana
yeye anaishi milele kuwaombea kwa Mungu.
26 Basi,
Yesu ndiye Kuhani Mkuu ambaye anatufaa sana katika mahitaji yetu. Yeye ni
mtakatifu, hana hatia wala dhambi ndani yake; hayumo katika kundi la wenye
dhambi na ameinuliwa mpaka juu mbinguni.
27 Yeye si
kama wale makuhani wakuu wengine; hana haja ya kutoa dhabihu kila siku, kwanza
kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Yeye
alifanya hivyo mara moja tu wakati alipojitoa yeye mwenyewe, na hiyo yatosha
kwa nyakati zote.
28 Sheria
ya Mose huwateua watu waliokuwa dhaifu kuwa makuhani wakuu; lakini ahadi ya
Mungu aliyoifanya kwa kiapo na ambayo imefika baada ya sheria imemteua Mwana
ambaye amefanywa mkamilifu milele.
|