Chapter 8
1 Basi,
jambo muhimu katika hayo tunayosema ni hili: sisi tunaye Kuhani Mkuu wa namna
hiyo, ambaye anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu
mbinguni.
2 Yeye
hutoa huduma ya Kuhani Mkuu katika Mahali Patakatifu sana, yaani ndani ya ile
hema ya kweli iliyojengwa na Bwana, siyo na binadamu. ic
3 Kila
Kuhani Mkuu ameteuliwa kumtolea Mungu vipawa na dhabihu, na hivyo Kuhani Mkuu
wetu lazima pia awe na kitu cha kutolea.
4 Kama
yeye angekuwa wa hapa duninani, asingekuwa kamwe kuhani, kwani wako makuhani
wengine wanaotoa sadaka kufuatana na Sheria.
5 Huduma
zao za kikuhani ni mfano tu na kivuli cha yale yaliyoko mbinguni. Ndivyo pia
ilivyokuwa kwa Mose. Wakati alipokuwa karibu kuitengeneza ile hema, Mungu
alimwambia: "Tengeneza kila kitu kufuatana na ule mfano ulioonyeshwa kule
mlimani."
6 Lakini
sasa Yesu amepewa huduma ya kikuhani iliyo bora zaidi kuliko yao, kama vile
agano alilothibitisha kati ya watu na Mungu ni bora zaidi, kwani lina msingi
wake katika ahadi za mambo yaliyo bora zaidi.
7 Maana
kama lile agano la kwanza halingalikuwa na dosari, hakungalikuwa na haja ya
agano la pili.
8 Lakini
Mungu aliwalaumu watu wake aliposema: "Siku zinakuja, asema Bwana, ambapo
nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na kabila la Yuda.
9 Agano
hili halitakuwa kama lile nililofanya na babu zao siku ile nilipowaongoza kwa
mkono kutoka nchi ya Misri. Hawakuwa waaminifu kwa agano langu; na hivyo mimi
sikuwajali, asema Bwana.
10 Na hili
ndilo agano nitakalofanya na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka
sheria zangu akilini mwao, na kuziandika mioyoni mwao. Mimi nitakuwa Mungu wao,
nao watakuwa watu wangu.
11 Hakuna
mtu atakayemfundisha mwananchi mwenzake, wala atakayemwambia ndugu yake: `Mjue
Bwana.` Maana watu wote, wadogo na wakubwa, watanijua mimi.
12
Nitawasamehe makosa yao, wala sitakumbuka tena dhambi zao."
13 Kwa
kusema juu ya agano jipya, Mungu alilichakaza lile la kwanza; na chochote
kinachochakaa na kuwa kikuukuu kitatoweka karibuni.
|