Chapter 9
1 Agano la
kwanza lilikuwa na taratibu zake za ibada na pia mahali patakatifu pa ibada
palipojengwa na watu.
2
Palitengenezwa hema ambayo sehemu yake ya nje iliitwa Mahali Patakatifu. Humo
mlikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyotolewa kwa Mungu.
3 Nyuma ya
pazia la pili, kulikuwa na hema iliyoitwa Mahali Patakatifu Kupita Pote.
4 Humo
mlikuwa na madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kufukizia ubani, na Sanduku la
Agano, ambalo lilikuwa limepakwa dhahabu pande zote, na ndani yake mlikuwa na
chungu cha dhahabu kilichokuwa na mana; fimbo ya Aroni iliyokuwa imechanua
majani, na vile vibao viwili vilivyoandikwa agano.
5 Juu ya
hilo Sanduku kulikuwa na viumbe vilivyodhihirisha kuweko kwa Mungu, na mabawa
yao yalitanda juu ya mahali ambapo dhambi huondolewa. Lakini sasa, hatuwezi
kusema kinaganaga juu ya mambo hayo.
6 Mipango
hiyo ilitekelezwa kisha ikawa desturi kwa makuhani kuingia kila siku katika
hema ya nje kutoa huduma zao.
7 Lakini
kuhani Mkuu peke yake ndiye anayeingia katika lile hema la pili; naye hufanya
hivyo mara moja tu kwa mwaka. Anapoingia ndani huwa amechukua damu ambayo
anamtolea Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi ambazo watu
wamezitenda bila wao wenyewe kujua.
8 Kutokana
na taratibu hizo Roho Mtakatifu anafundisha wazi kwamba wakati ile hema ya nje
ingali ipo imesimama, njia ya kuingia Mahali Patakatifu haijafunguliwa.
9 Jambo hili
ni mfano wa nyakati za sasa. Linaonyesha kwamba zawadi na dhabihu zinazotolewa
kwa Mungu haziwezi kuifanya mioyo ya wale wanaoabudu kuwa mikamilifu,
10 kwani
haya yote yanahusika na vyakula, vinywaji na taratibu mbalimbali za kutawadha.
Yote hayo ni maagizo ya njenje tu; na nguvu yake hukoma wakati Mungu
atakaporekebisha vitu vyote.
11 Lakini
Kristo amekwisha fika, akiwa Kuhani Mkuu wa mambo yaliyo mema, ambayo sasa
yamekwisha fika. Yeye anatoa huduma zake katika hema iliyo bora na kamilifu
zaidi, isiyofanywa kwa mikono ya watu, yaani isiyo ya ulimwengu huu ulioumbwa.
12 Yeye
aliingia Mahali Patakatifu mara moja tu, tena hakuwa amechukua damu ya mbuzi
wala ng`ombe, bali aliingia kwa damu yake yeye mwenyewe, akatupatia ukombozi wa
milele.
13 Watu
waliokuwa najisi kidini waliweza kutakasika na kuwa safi waliponyunyiziwa damu
ya mbuzi na ya ng`ombe pamoja na majivu ya ndama.
14 Lakini,
kwa damu ya Kristo, mambo makuu zaidi hufanyika! Kwa nguvu za Roho wa milele,
Kristo alijitolea mwenyewe dhabihu kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa
dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo kifo, ili tupate kumtumikia Mungu
aliye hai.
15 Kwa
hiyo, Kristo ndiye aliyeratibisha agano jipya ili wale walioitwa na Mungu
wazipokee baraka za milele walizoahidiwa. Watazipata, kwani kifo kimetokea
ambacho huwakomboa watu kutoka yale makosa waliyofanya wakati wa lile agano la
kale.
16 Kwa
kawaida wosia hutambuliwa tu kama kifo cha yule aliyeufanya huo wosia
kimethibitishwa.
17 Wosia
hauwezi kutekelezwa mpaka kumetokea kifo, kwani wosia hauna maana ikiwa mwenye
kuufanya bado anaishi.
18 Ndiyo
maana hata lile agano la kwanza halikuwekwa bila damu kumwagwa.
19 Kwanza
Mose aliwatangazia watu wote amri zote kama ilivyokuwa katika Sheria; kisha
akachukua damu ya ndama pamoja na maji, na kwa kutumia majani ya mti uitwao
husopo na pamba nyekundu, akakinyunyizia kile kitabu cha Sheria na hao watu
wote.
20 Mose
alisema: "Hii ni damu inayothibitisha agano mliloamriwa na Mungu
mlitii."
21
Vilevile Mose aliinyunyizia damu ile hema na vyombo vya ibada.
22 Naam,
kadiri ya Sheria karibu kila kitu chaweza kutakaswa kwa damu, na dhambi nazo
zaondolewa tu ikiwa damu imemwagwa.
23 Vitu
hivi ambavyo ni mfano tu wa mambo halisi ya mbinguni, vililazimika kutakaswa
kwa namna hiyo. Lakini vitu vya mbinguni huhitaji dhabihu iliyo bora zaidi.
24 Maana
Kristo hakuingia Mahali Patakatifu palipojengwa kwa mikono ya watu, ambapo ni
mfano tu wa kile kilicho halisi. yeye aliingia mbinguni kwenyewe ambako sasa
anasimama mbele ya Mungu kwa ajili yetu.
25 Kuhani
Mkuu wa Wayahudi huingia Mahali Patakatifu kila mwaka akiwa amechukua damu ya
mnyama; lakini Kristo hakuingia humo ili ajitoe mwenyewe mara nyingi,
26 maana
ingalikuwa hivyo, Kristo angalipaswa kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa
ulimwengu. Lakini sasa nyakati hizi zinapokaribia mwisho wake, yeye ametokea
mara moja tu, kuondoa dhambi kwa kujitoa yeye mwenyewe dhabihu.
27 Basi,
kama vile kila mtu hufa mara moja tu, kisha husimama mbele ya hukumu ya Mungu,
28 vivyo
hivyo Kristo naye alijitoa dhabihu mara moja tu kwa ajili ya kuziondoa dhambi
za wengi. Atakapotokea mara ya pili si kwa ajili ya kupambana na dhambi, bali
ni kwa ajili ya kuwaokoa wale wanaomngojea.
|