Chapter 10
1 Sheria
ya Wayahudi si picha kamili ya mambo yale halisi: ni kivuli tu cha mema
yanayokuja. Dhabihu zilezile hutolewa daima, mwaka baada ya mwaka. Sheria yawezaje,
basi, kwa njia ya dhabihu hizo, kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu?
2 Kama hao
watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia
tena kuwa na dhambi, na dhabihu hizo zote zingekoma.
3 Lakini
dhabihu hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao.
4 Maana
damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi.
5 Ndiyo
maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: "Hukutaka dhabihu
wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili.
6 Sadaka
za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi.
7 Hapo
nikasema: `Niko hapa ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako kama ilivyoandikwa
juu yangu katika kitabu cha Sheria."`
8 Kwanza
alisema: "Hutaki, wala hupendezwi na dhabihu na sadaka, sadaka za
kuteketezwa na za kuondoa dhambi." Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote
hutolewa kufuatana na Sheria.
9 Kisha
akasema: "Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako." Hivyo
Mungu alibatilisha dhabihu za zamani na mahali pake akaweka dhabihu nyingine
moja.
10 Kwa
kuwa Yesu Kristo alitimiza mapenzi ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa
ile dhabihu ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha.
11 Kila
kuhani Myahudi humhudumia Mungu kila siku, akitoa dhabibu zilezile mara nyingi,
dhabibu ambazo haziwezi kuondoa dhambi.
12 Lakini
Kristo alitoa dhabihu moja tu kwa ajili ya dhambi, dhabihu ifaayo milele, kisha
akaketi upande wa kulia wa Mungu.
13 Huko
anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake.
14 Basi,
kwa dhabihu yake moja tu, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa
dhambi zao.
15 Naye
Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema:
16
"Hili ndilo agano nitakalofanya nao, katika siku zijazo, asema Bwana:
Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao."
17 Kisha
akaongeza kusema: "Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya
uhalifu."
18 Basi,
dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa dhabihu za kuondoa
dhambi.
19 Basi,
ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu.
20 Yeye
ametufungulia njia mpya na yenye uzima kupitia lile pazia, yaani kwa njia ya
mwili wake mwenyewe.
21 Basi,
tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu.
22 Kwa
hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa
dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi.
23
Tushikilie imara tumaini lile tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni
mwaminifu.
24
Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na
kutenda mema.
25
Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali
tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, Siku ile ya Bwana inakaribia.
26 Maana,
tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kufahamu ukweli, hakuna dhabihu
iwezayo kutolewa tena kwa ajili ya kuondoa dhambi.
27
Linalobaki ni kungojea tu kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali
utakaowaangamiza wote wanaompinga.
28 Mtu
yeyote asiyeitii Sheria ya Mose, huuawa bila ya huruma kukiwa na ushahidi wa
watu wawili au watatu.
29 Je, mtu
yule anayempuuza Mwana wa Mungu na kuidharau damu ya agano la Mungu
iliyomtakasa, mtu anayemtukana Roho wa Mungu, anastahili kupata adhabu kali ya
namna gani?
30 Maana
tunamfahamu yule aliyesema, "Mimi nitalipiza kisasi, mimi
nitalipiza," na ambaye alisema pia, "Bwana atawahukumu watu
wake."
31
Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha mno!
32
Kumbukeni yaliyotokea siku zile za kwanza mlipoangaziwa mwanga wa Mungu. Ingawa
siku zile mlipatwa na mateso mengi, ninyi mlistahimili.
33 Mara
nyingine mlitukanwa na kufedheheshwa hadharani; mara nyingine mlikuwa radhi
kuungana na wale walioteswa namna hiyohiyo.
34
Mlishiriki mateso ya wafungwa, na mliponyang`anywa mali yenu mlistahimili kwa
furaha, maana mlijua kwamba mnayo mali bora zaidi na ya kudumu milele.
35 Basi,
msipoteze uhodari wenu, maana utawapatieni tuzo kubwa.
36
Mnahitaji kuwa na uvumilivu, ili mweze kufanya anayotaka Mungu na kupokea kile
alichoahidi.
37 Maana
kama yasemavyo Maandiko: "Bado kidogo tu, na yule anayekuja, atakuja, wala
hatakawia.
38 Lakini
mtu wangu aliye mwadilifu ataamini na kuishi; walakini akirudi nyuma, mimi
sitapendezwa naye."
39 Basi,
sisi hatumo miongoni mwa wale wanaorudi nyuma na kupotea, ila sisi tunaamini na
tunaokolewa.
|