Chapter 12
1 Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa
hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotung`ang`ania.
Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu.
2 Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na
ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia
kifo msalabani, bila kujali juu ya aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia
wa kiti cha enzi cha Mungu.
3 Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi
alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala
msikate tamaa.
4 Maana katika kupambana na dhambi, ninyi hamjapigana mpaka
kiasi cha kumwaga damu yenu.
5 Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu
anawataja ninyi kuwa wanawe? "Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala
usife moyo anapokukanya.
6 Maana Bwana humwadhibu kila anayempenda, humpinga kila
anayekubali kuwa mwanae."
7 Vumilieni adhabu kwani ni mafundisho; Mungu huwatendea
ninyi kama wanawe. Maana ni mwana gani asiyeadhibiwa na baba yake?
8 Lakini msipoadhibiwa kama wana wengine, basi, ninyi si
wanawe, bali ni wana haramu.
9 Zaidi ya hayo sisi tunawaheshimu wazazi wetu waliotuzaa
hata wanapotuadhibu. Basi, tunapaswa kumtii zaidi Baba yetu wa kiroho ili
tupate kuishi.
10 Wazazi wetu hapa duniani walituadhibu kwa muda, kama wao
wenyewe walivyoona kuwa vema; lakini Mungu anatuadhibu kwa ajili ya faida yetu
wenyewe, tupate kuushiriki utakatifu wake.
11 Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha.
Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka
katika maisha adili!
12 Basi, inueni mikono yenu inayolegea na kuimarisha magoti
yenu yaliyo dhaifu.
13 Endeleeni kutembea katika njia iliyonyoka, ili kile
kilicholemaa kisiumizwe, bali kiponywe.
14 Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote. Ishini maisha
ya utakatifu, kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Bwana bila ya maisha kama
hayo.
15 Jitahidini sana mtu yeyote asije akapoteza neema ya
Mungu. Muwe waangalifu ili mti mchungu usizuke kati yenu na kuwaua wengi kwa
sumu yake.
16 Jihadharini ili miongoni mwenu pasiwe na mtu mwasherati
au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, aliyeuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa
mlo mmoja.
17 Ninyi mnafahamu kwamba hata alipotaka kuipata tena ile
baraka iliyokuwa yake, alikataliwa, maana hakupata tena nafasi ya kutubu,
ingawa aliitafuta kwa machozi.
18 Ninyi hamkuwasili mlimani Sinai, ambao unaweza kushikika
kama walivyofanya watu wa Israeli, hamkufika kwenye moto uwakao, penye giza,
tufani,
19 mvumo wa tarumbeta na sauti ya maneno. Wale waliosikia
sauti hiyo waliomba wasisikie tena neno jingine,
20 kwani hawakuweza kustahimili amri iliyotolewa:
"Atakayegusa mlima huu, hata kama ni mnyama, atapigwa mawe."
21 Hayo yote yalionekana ya kutisha mno, hata Mose akasema,
"Naogopa na kutetemeka."
22 Lakini ninyi mmefika katika mlima wa Sioni, kwenye mji
wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni, ambapo wamekusanyika
malaika elfu nyingi wasiohesabika.
23 Mmefika kwenye kusanyiko kubwa la wazaliwa wa kwanza wa
Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mnasimama mbele ya Mungu aliye
hakimu wa wote, na mbele ya roho za watu waadilifu waliofanywa kuwa wakamilifu.
24 Mmefika kwa Yesu ambaye ameratibisha agano jipya, na
ambaye damu yake iliyomwagika inasema mambo mema zaidi kuliko ile ya Abeli.
25 Basi, jihadharini msije mkakataa kumsikiliza yeye ambaye
anasema nanyi. Kama wale walikataa kumsikiliza yule aliyewaonya hapa duniani
hawakuokoka, sisi tutawezaje kuokoka kama tukikataa kumsikiliza yule
anayetuonya kutoka mbinguni?
26 Wakati ule sauti ilitetemesha nchi, lakini sasa
ameahidi: "Nitatetemesha nchi tena, lakini si nchi tu bali pia
mbingu."
27 Neno hili: "tena" linatuonyesha kwamba vitu
vyote vilivyoumbwa vitatetemeshwa na kutoweka ili vibaki vile
visivyotetemeshwa.
28 Sisi basi, na tushukuru kwani tunapokea utawala
usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza,
kwa ibada na hofu;
29 maana Mungu wetu kweli ni moto mkali unaoteketeza.
|