James
Chapter 1
1 Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo,
nawaandikia ninyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salaam!
2 Ndugu
zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali,
3 kwani
mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu.
4 Muwe na
hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu
na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.
5 Lakini
kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye
atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.
6 Lakini
anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama
mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo.
7 Mtu wa
namna hiyo, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote,
asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.
8 []
9 Ndugu
aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza,
10 naye
tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua
la porini.
11 Jua
huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na
uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli
zake.
12 Heri
mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili atapewa tuzo la
uzima ambalo Mungu aliwaahidia wale wanaompenda.
13 Kama
mtu akijaribiwa, asiseme: "Ninajaribiwa na Mungu." Maana Mungu hawezi
kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote.
14 Lakini
mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya.
15 Tamaa
ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo.
16 Ndugu
zangu wapenzi, msidanganyike!
17 Kila
kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba
wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu.
18 Kwa
kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe namna ya matunda
ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.
19 Ndugu
zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini
asiwe mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika.
20 Mwenye
hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki.
21 Kwa
hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya
Mungu na kupokea ule ujumbe uliopandwa mioyoni mwenu, ambao waweza kuziokoa
nafsi zenu.
22
Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa
vitendo.
23 Yeyote
anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia
sura yake mwenyewe katika kioo.
24
Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo.
25 Lakini
mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu
anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali
anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya.
26 Kama
mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini
yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe.
27 Dini
iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima
na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu
huu.
|