Chapter 2
1 Ndugu
zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu
kamwe.
2 Tuseme
mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika
mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu.
3 Ikiwa
mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: "Keti hapa
mahali pazuri," na kumwambia yule maskini: "Wewe, simama huko,"
au "Keti hapa sakafuni miguuni pangu,"
4 je, huo
si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya?
5 Ndugu
zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika
ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea Utawala
aliowaahidia wale wanaompenda.
6 Lakini
ninyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamizeni na
kuwapeleka mahakamani?
7 Je, si
haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa?
8 Kama
mnaitimiza ile sheria ya Utawala kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu:
"Mpende binadamu mwenzako kama unavyojipenda wewe mwenyewe", mtakuwa
mnafanya vema kabisa.
9 Lakini
mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo Sheria inawahukumu ninyi kuwa mna
hatia.
10 Anayevunja
amri mojawapo ya Sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja Sheria yote.
11 Maana
yuleyule aliyesema: "Usizini," alisema pia "Usiue". Kwa
hiyo, hata ikiwa hukuzini lakini umeua, wewe umeivunja Sheria.
12 Basi,
semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru.
13 Maana,
Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma
hushinda hukumu.
14 Ndugu
zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je,
hiyo imani yawezaje kumwokoa?
15 Tuseme
kaka au dada hana nguo au chakula.
16 Yafaa
kitu gani ninyi kuwaambia hao: "Nendeni salama mkaote moto na
kushiba," bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha?
17 Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa.
18 Lakini mtu anaweza kusema: "Wewe unayo imani, mimi
ninayo matendo!" Haya! Nionyeshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila
matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu.
19 Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini
hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu.
20 Mpumbavu wee! Je, wataka kuonyeshwa kwamba imani bila
matendo imekufa?
21 Je, Abrahamu baba yetu alipataje kukubalika mbele yake
Mungu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa mwanae Isaka sadaka juu ya madhabahu.
22 Waona basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo
yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake.
23 Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo:
"Abrahamu alimwamini Mungu na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu
mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki wa Mungu."
24 Mnaona basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa
matendo yake na si kwa imani peke yake.
25 Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye
alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia
waende zao kwa kupitia njia nyingine.
26 Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo
imani bila matendo imekufa.
|