Chapter 3
1 Ndugu zangu, wengi wenu msiwe walimu. Kama mjuavyo, sisi
walimu tutapata hukumu kubwa zaidi kuliko wengine.
2 Lakini kama mtu hakosi katika usemi wake, basi, huyo ni
mkamilifu, na anaweza kutawala nafsi yake yote.
3 Sisi huwatia farasi lijamu kinywani mwao ili watutii; na
kwa njia hiyo twaweza kuwaongoza kokote tunakotaka.
4 Meli nazo pia, ingawa ni kubwa sana, na husukumwa na
upepo mkali, huweza kugeuzwa kwa usukani mdogo sana, zikaelekea kokote nahodha
anakotaka.
5 Vivyo hivyo, ulimi, ingawa ni kiungo kidogo cha mwili,
hujisifia makuu sana. ic Moto mdogo waweza kuteketeza msitu mkubwa.
6 Hali kadhalika ulimi ni kama moto. Umejaa maovu chungu
nzima, unayo nafasi yake katika miili yetu na hueneza ubaya katika nafsi zetu
zote. Huteketeza maisha yetu yote kwa moto utokao Jehanamu kwenyewe.
7 Binadamu anaweza kuwafuga wanyama, na amefaulu kufuga
viumbe vyote-wanyama wa mwituni, ndege, nyoka na viumbe vya baharini.
8 Lakini hakuna mtu aliyeweza kuufuga ulimi. Ulimi ni kitu
kiovu, hakitawaliki, na kimejaa sumu inayoua.
9 Kwa ulimi sisi twamshukuru Bwana na Baba yetu. Kwa ulimi
huohuo twawalaani watu, watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu.
10 Maneno ya laana na ya kusifia hutoka katika kinywa
kimoja. Ndugu zangu, mambo haya hayapaswi kuwa hivyo.
11 Je, chemchemi moja yaweza kutoa maji matamu na maji
machungu pamoja?
12 Ndugu zangu, je, mti wa mtini waweza kuzaa zeituni? Au,
mzabibu waweza kuzaa tini? Chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji
matamu.
13 Je, ni nani mwenye hekima na akili miongoni mwenu? Basi,
aonyeshe jambo hilo kwa mwenendo wake mzuri na kwa matendo yake mema
yanayofanyika kwa unyenyekevu na hekima.
14 Lakini ikiwa mioyo yenu imejaa wivu, chuki na ubinafsi,
basi, msijisifu na kusema uongo dhidi ya ukweli.
15 Hekima ya namna hiyo haitoki juu mbinguni; hekima hiyo
ni ya ulimwengu, na ya kidunia, tena ni ya kishetani.
16 Maana
popote palipo na wivu na ubinafsi hapo pana fujo na kila aina ya uovu.
17 Lakini
hekima itokayo juu mbinguni, kwanza ni safi; inapenda amani, upole na huwajali
watu; imejaa huruma na huzaa matunda ya matendo mema; haina ubaguzi wala
unafiki.
18
Uadilifu ni mazao ya mbegu ambazo wapenda amani hupanda katika amani.
|