Chapter 4
1 Mapigano
na magombano yote kati yenu yanatoka wapi? Hutoka katika tamaa zenu mbaya
ambazo hupigana daima ndani yenu.
2
Mnatamani vitu na kwa vile hamvipati mko tayari kuua; mwatamani sana kupata
vitu, lakini hamvipati, hivyo mnagombana na kupigana. Hampati kile mnachotaka
kwa sababu hamkiombi kwa Mungu.
3 Tena,
mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate
kutosheleza tamaa zenu.
4 Ninyi ni
watu msio na uaminifu kama wazinzi. Je, hamjui kwamba kuwa rafiki wa ulimwengu
ni kuwa adui wa Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa ulimwengu anajifanya
adui wa Mungu.
5
Msifikiri kwamba Maandiko Matakatifu yamesema maneno ya bure, yanaposema:
"Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu ana wivu mkubwa."
6 Lakini,
neema tunayopewa na Mungu ina nguvu zaidi; kama yasemavyo Maandiko: "Mungu
huwapinga wenye majivuno lakini huwapa neema wanyenyekevu."
7 Basi,
jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Ibilisi naye atawakimbieni.
8 Mkaribieni
Mungu, naye atakuja karibu nanyi. Osheni mikono yenu enyi wakosefu! Safisheni
mioyo yenu enyi wanafiki!
9 Oneni
huzuni, lieni na kuomboleza; kicheko chenu na kiwe kilio; na furaha yenu iwe
huzuni kubwa.
10
Nyenyekeeni mbele ya Bwana, naye atawainueni.
11 Ndugu,
msilaumiane ninyi kwa ninyi. Anayemlaumu ndugu yake na kumhukumu, huyo huilaumu
na kuihukumu Sheria. Kama ukiihukumu Sheria, basi, wewe huitii Sheria, bali
waihukumu.
12 Mungu peke
yake ndiye mwenye kuweka Sheria na kuhukumu. Ni yeye peke yake anayeweza kuokoa
na kuangamiza. Basi, wewe ni nani hata umhukumu binadamu mwenzako?
13 Basi,
sasa sikilizeni ninyi mnaosema: "Leo au kesho tutakwenda katika mji fulani
na kukaa huko mwaka mzima tukifanya biashara na kupata faida."
14 Ninyi
hamjui hata maisha yenu yatakavyokuwa kesho! Ninyi ni kama ukungu unaotokea kwa
muda mfupi tu na kutoweka tena.
15
Mngalipaswa kusema: "Bwana akitujalia tutaishi na tutafanya hiki au
kile."
16 Lakini
sasa mwajivuna na kujigamba; majivuno ya namna hiyo ni mabaya.
17 Basi,
mtu ambaye hafanyi lile jambo jema analojua kwamba anapaswa kulifanya, anatenda
dhambi.
|