Chapter 5
1 Na sasa
sikilizeni enyi matajiri! Lieni na kuomboleza kwa sababu ya taabu
zitakazowajieni.
2 Mali
zenu zimeoza, na nguo zenu zimeliwa na nondo.
3 Dhahabu yenu
na fedha vimeota kutu, na kutu hiyo itakuwa ushahidi dhidi yenu, nayo itakula
miili yenu kama vile moto. Ninyi mmejilundikia mali katika siku hizi za mwisho!
4
Hamkuwalipa mishahara watumishi waliofanya kazi katika mashamba yenu. Sikilizeni
malalamiko yao! Kilio cha hao wanaovuna mashamba yenu kimefika masikioni mwa
Bwana, Mwenye Nguvu.
5 Mmeishi
duniani maisha ya kujifurahisha na ya anasa. Mmejinenepesha tayari kwa siku ya
kuchinjwa.
6
Mmemhukumu na kumwua mtu asiye na hatia, naye hakuwapigeni.
7 Basi,
ndugu zangu, muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja. Tazameni mkulima
anavyongoja kwa subira mimea yake itoe mavuno mazuri. Yeye hungojea kwa subira
mvua za masika na za vuli.
8 Nanyi
pia mnapaswa kuwa na subira; imarisheni mioyo yenu, maana siku ya kuja kwake
Bwana inakaribia.
9 Ndugu
zangu, msinung`unikiane ninyi kwa ninyi msije mkahukumiwa na Mungu. Hakimu yu
karibu, tayari kuingia.
10 Ndugu,
mkitaka kuona mfano wa subira na uvumilivu katika mateso, fikirini juu ya
manabii ambao walinena kwa jina la Bwana.
11
Tunawaita hao wenye heri kwa sababu walivumilia. Mmesikia habari za uvumilivu
wa Yobu, na mnajua jinsi Bwana alivyomtendea mwishoni. Maana Bwana amejaa
huruma na rehema.
12 Zaidi
ya hayo yote, ndugu zangu, msiape kwa mbingu, wala kwa dunia, wala kwa kitu
kingine chochote. Semeni "Ndiyo" kama maana yenu ni ndiyo, na
"La" kama maana yenu ni la, na hapo hamtahukumiwa na Mungu.
13 Je,
pana mtu yeyote miongoni mwenu aliye na shida? Anapaswa kusali. Je, yuko mwenye
furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa.
14 Je,
yuko mgonjwa kati yenu? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa, nao watamwombea na
kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.
15
Wakiomba kwa imani mgonjwa ataponyeshwa; Bwana atampatia nafuu, na dhambi
alizotenda zitaondolewa.
16 Basi, ungamanianeni dhambi zenu, na ombeaneni, ili mpate
kuponywa. Sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda mengi.
17 Eliya alikuwa binadamu kama sisi. Aliomba kwa moyo mvua
isinyeshe, nayo haikunyesha nchini kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita.
18 Kisha akaomba tena, mvua ikanyesha kutoka angani na nchi
ikatoa mazao yake.
19 Ndugu zangu, mmoja wenu akipotoka kuhusu ukweli, na
mwingine akamrudisha,
20 fahamuni kwamba, huyo anayemrudisha mwenye dhambi kutoka
njia yake ya upotovu, ataiokoa roho yake kutoka kifo, na dhambi nyingi
zitaondolewa.
|