1 Peter
Chapter 1
1 Mimi Petro, mtume wa Yesu Kristo nawaandikia ninyi
wateule wa Mungu Baba, ambao mmetawanyika na mnaishi kama wakimbizi huko Ponto,
Galatia, Kapadokia, Asia na Bithunia.
2 Mungu Baba aliwateua ninyi kufuatana na kusudi lake, na
mmefanywa watakatifu na Roho, mpate kumtii Yesu Kristo na kusafishwa kwa damu
yake. Nawatakieni neema na amani tele.
3 Asifiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa
huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka wafu.
Ametujalia tumaini lenye uzima,
4 na hivyo tunatazamia kupata baraka zile ambazo Mungu
aliwawekea watu wake. Mungu amewawekeeni baraka hizo mbinguni ambako haziwezi
kuoza au kuharibika au kufifia.
5 Hizo zitakuwa zenu ninyi ambao kwa imani mnalindwa salama
kwa nguvu ya Mungu kwa ajili ya wokovu ambao uko tayari kufunuliwa mwishoni mwa
nyakati.
6 Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo
kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka.
7 Shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu
yenyewe ambayo huharibika, hujaribiwa kwa moto; hali kadhalika na imani yenu
ambayo ni ya thamani zaidi kuliko dhahabu, ni lazima ijaribiwe ipate kuwa
thabiti. Hapo mtapokea sifa na utukufu na heshima Siku ile Yesu Kristo
atakapofunuliwa.
8 Ninyi mnampenda ingawaje hamjamwona, na mnamwamini ingawa
hamumwoni sasa. Hivyo, mnafurahi kwa furaha tukufu isiyoelezeka,
9 kwa sababu mnapokea wokovu wa roho zenu ambao ni lengo la
imani yenu.
10 Manabii walipeleleza kwa makini na kufanya uchunguzi juu
ya wokovu huo, wakabashiri juu ya neema hiyo ambayo ninyi mngepewa.
11 Walijaribu kujua nyakati na mazingira ya tukio hilo,
yaani wakati alioudokezea Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, akibashiri juu ya
mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaofuata.
12 Mungu aliwafunulia kwamba wakati walipokuwa wanasema juu
ya hayo mambo ambayo ninyi mmekwisha sikia sasa kutoka kwa wale wajumbe
waliowatangazieni Habari Njema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka
mbinguni, hiyo kazi yao haikuwa kwa faida yao wenyewe, bali kwa ajili yenu.
Hayo ndiyo mambo ambayo hata malaika wangependa kuyafahamu.
13 Kwa hiyo, basi, muwe tayari kabisa kwa nia, na kukesha.
Wekeni tumaini lenu lote katika baraka ile mtakayopewa wakati Yesu Kristo
atakapoonekana!
14 Kama watoto wa Mungu wenye utii, msikubali kamwe kufuata
tena tamaa mbaya mlizokuwa nazo wakati mlipokuwa wajinga.
15 Bali mnapaswa kuwa watakatifu katika mwenendo wenu wote,
kama vile yule aliyewaiteni ni mtakatifu.
16 Maandiko yasema: "Muwe watakatifu, kwa kuwa mimi ni
mtakatifu."
17 Mnapomtaja Mungu ninyi humwita Baba. Basi, jueni kwamba
yeye humhukumu kila mmoja kadiri ya matendo yake, bila ubaguzi. Hivyo tumieni
wakati wenu uliowabakia hapa ugenini katika kumcha Mungu.
18 Maana mnajua kwamba ninyi mlikombolewa katika mwenendo
wenu usiofaa ambao mliupokea kutoka kwa wazee wenu, si kwa vitu vyenye
kuharibika: kwa fedha na dhahabu;
19 bali mlikombolewa kwa damu tukufu ya Kristo, ambaye
alikuwa kama mwana kondoo asiye na dosari wala doa.
20 Yeye alikuwa ameteuliwa na Mungu kabla ya ulimwengu
kuumbwa, akafunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu.
21 Kwa njia yake, ninyi mnamwamini Mungu aliyemfufua kutoka
wafu na kumpa utukufu; na hivyo imani na matumaini yenu yako kwa Mungu.
22 Maadamu sasa, kwa kuutii ukweli, ninyi mmezitakasa roho
zenu na kuwapenda wenzenu bila unafiki, basi, pendaneni kwa moyo wote.
23 Maana kwa njia ya neno hai la Mungu, ninyi mmezaliwa
upya, si kama watoto wa baba awezaye kufa, bali baba asiyekufa milele.
24 Kama Maandiko yasemavyo: "Kila binadamu ni kama
nyasi, na utukufu wake wote ni kama maua ya porini. Nyasi hunyauka na maua
huanguka.
25 Lakini neno la Bwana hudumu milele." Neno hilo ni
hiyo Habari Njema iliyohubiriwa kwenu.
|