Chapter 2
1 Basi, acheni uovu wote; uongo, unafiki, wivu na maneno ya
kashfa visiweko tena.
2 Kama vile watoto wachanga wanavyotamani maziwa, nanyi pia
mnapaswa kuwa na hamu ya maziwa halisi ya kiroho, ili kwa nguvu yake mpate
kukua na kukombolewa.
3 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mmegundua
kwamba Bwana ni mwema."
4 Basi, mwendeeni Bwana! Yeye ndiye jiwe hai lililokataliwa
na watu; lakini mbele ya Mungu ni jiwe teule, na la thamani kubwa.
5 Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya
kiroho, ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea dhabihu za kiroho
zenye kumpendeza Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.
6 Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Tazama! Naweka
huko sioni jiwe kuu la msingi, jiwe la thamani kubwa nililoliteua. Mtu
atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa."
7 Kwenu ninyi mnaoamini, jiwe hilo ni la thamani kubwa;
lakini kwa wale wasioamini, "Jiwe walilokataa waashi, sasa limekuwa jiwe
kuu la msingi."
8 Tena Maandiko yasema: "Jiwe hilo ni jiwe la
kujikwaa, mwamba wa kuwaangusha watu." Watu hujikwaa kwa sababu hawauamini
ule ujumbe; na ndivyo walivyopangiwa tangu mwanzo.
9 Lakini ninyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa
takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya
Mungu aliyewaiteni kutoka gizani akawaingizeni katika mwanga wake mkuu.
10 Wakati mmoja ninyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa
ninyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa
mmeipokea.
11 Wapenzi wangu, nawasihi ninyi kama wageni na wakimbizi
hapa duniani! Achaneni na tamaa za mwili ambazo hupingana na roho.
12 Mwenendo wenu kati ya watu wasiomjua Mungu unapaswa kuwa
mwema kabisa, ili hata watakapowasingizieni kwamba mnatenda mabaya, waweze
kutambua matendo yenu mema na hivyo wamtukuze Mungu Siku ya kuja kwake.
13 Basi, jiwekeni chini ya mamlaka yote ya kibinadamu, kwa
ajili ya Bwana: utii kwa mfalme aliye mtawala mkuu,
14 utii kwa wakuu wa mikoa ambao wameteuliwa naye
kuwaadhibu wahalifu na kuwasifu watendao mema.
15 Maana Mungu anataka mweze kuyakomesha maneno ya kijinga
ya watu wasio na akili kwa matendo mema mnayofanya.
16 Ishini kama watu huru; lakini msiutumie uhuru wenu
kuuficha ubaya, bali ishini kama watumishi wa Mungu.
17 Waheshimuni watu wote, wapendeni ndugu zenu waumini,
mcheni Mungu, mheshimuni mfalme.
18 Enyi watumishi wa nyumbani, watiini wakuu wenu kwa
heshima yote, wawe wema na wapole au wenye kuchukiza.
19 Maana kama mnavumilia maumivu ya mateso msiyostahili kwa
sababu mwajua kwamba Mungu anataka hivyo, basi Mungu atawafadhili.
20 Maana, mtapata tuzo gani mkivumilia mapigo mnayostahili
kwa sababu ya makosa yenu? Lakini kama mnavumilia mateso hata ingawa mmetenda
mema, Mungu atawapeni baraka kwa ajili hiyo.
21 Hayo ndiyo mliyoitiwa; maana Kristo mwenyewe aliteseka
kwa ajili yenu, akawaachieni mfano, ili muufuate mwenendo wake.
22 Yeye hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu
halikusikika mdomoni mwake.
23 Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye
hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki.
24 Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake
juu ya msalaba, tupate kufa kuhusu dhambi, na kuishi kwa ajili ya uadilifu. Kwa
majeraha yake, ninyi mmeponywa.
25 Ninyi mlikuwa kama kondoo waliokuwa wamepotea; lakini
sasa mmemrudia Mchungaji na Mlinzi wa roho zenu.
|