Chapter 4
1 Maadamu
Kristo aliteseka kimwili, nanyi pia mnapaswa kujiimarisha kwa nia hiyo yake;
maana mtu akisha teseka kimwili hahusiki tena na dhambi.
2 Tangu
sasa, basi, maisha yaliowabakia kuishi hapa duniani yanapaswa kuongozwa na
matakwa ya Mungu, si na tamaa za kibinadamu.
3 Wakati
uliopita mlikuwa na muda mrefu wa kufanya mambo wanayofanya watu wasiomjua
Mungu. Mliishi maisha ya anasa, ubinafsi, ulevi, ugomvi, kunywa mno na ya ibada
haramu za sanamu.
4 Sasa,
watu hao wasiomjua Mungu wanashangaa wanapoona kwamba hamwandamani nao tena
katika hali ya kuishi vibaya, na hivyo wanawatukaneni.
5 Lakini
watapaswa kutoa hoja juu ya jambo hilo mbele yake Mungu aliye tayari kuwahukumu
wazima na wafu!
6 Kwa
sababu hiyo, hao waliokufa ambao walikuwa wamehukumiwa katika maisha yao ya
kimwili kama anavyohukumiwa kila mmoja, walihubiriwa Habari Njema kusudi katika
maisha yao ya kiroho waishi kama aishivyo Mungu.
7 Mwisho
wa vitu vyote umekaribia. Kwa hiyo mnapaswa kuwa na utaratibu na nidhamu, ili
mweze kusali.
8 Zaidi ya
yote pendaneni kwa moyo wote, maana upendo hufunika dhambi nyingi.
9 Muwe na
ukarimu ninyi kwa ninyi bila kunung`unika.
10 Kila
mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine, kama
vile uwakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu.
11
Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumika anapaswa
kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe
kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele!
Amina.
12 Wapenzi
wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na
kitu kisicho cha kawaida.
13 Ila
furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili mweze kuwa na furaha tele
wakati utukufu wake utakapofunuliwa.
14 Heri
yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha
kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa juu yetu.
15 Asiwepo
mtu yeyote miongoni mwenu ambaye anapaswa kuteseka kwa sababu ni muuaji, mwizi,
mhalifu au mwovu.
16 Lakini
kama mtu akiteseka kwa sababu ni Mkristo, basi asione aibu, bali amtukuze
Mungu, kwa sababu mtu huyo anaitwa kwa jina la Kristo.
17 Wakati
wa hukumu umefika, na hukumu hiyo inaanza na watu wake Mungu mwenyewe. Ikiwa
hukumu hiyo inaanzia kwetu sisi, basi mwisho wake utakuwa namna gani kwa wale
wasioamini Habari Njema ya Mungu?
18 Kama
yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni vigumu kwa watu waadilifu kuokolewa;
itakuwaje basi kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi?"
19 Kwa
hiyo, wale wanaoteseka kufuatana na matakwa ya Mungu, wanapaswa, kwa matendo
yao mema, kujiweka chini ya Muumba wao ambaye ni wa kuaminika kabisa.
|