2 Peter
Chapter 1
1 Mimi
Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia ninyi ambao, kwa
wema wake Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo, mmejaliwa imani ileile ya thamani
kuu tuliyojaliwa sisi.
2 Nawatakieni
neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.
3 Kwa
uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji, ili tuishi
maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema
wake yeye mwenyewe.
4 Kwa
namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa
zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na mpate
kuishiriki hali yake ya kimungu.
5 Kwa
sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza fadhila katika imani yenu: ongezeni
elimu katika fadhila yenu,
6 kuwa na
kiasi katika elimu yenu, uvumilivu katika kuwa na kiasi, uchaji wa Mungu katika
uvumilivu wenu,
7 udugu
katika uchaji wenu, na mapendo katika udugu wenu.
8 Mkiwa na
sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika
kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
9 Lakini
mtu asiye na sifa hizo ni kipofu, hawezi kuona na amesahau kwamba alikwisha
takaswa dhambi zake za zamani.
10 Kwa
hiyo basi, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na
Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo
hamtaanguka kamwe.
11 Kwa
namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika Utawala wa milele wa
Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
12 Kwa
hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu, na
mko imara katika ukweli mlioupokea.
13 Nadhani
ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na
kuwakumbusheni juu ya mambo haya.
14 Najua
kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia
waziwazi.
15 Basi,
nitajitahidi kuwapatieni njia ya kuyakumbuka mambo haya kila wakati, baada ya
kufariki kwangu.
16 Wakati
tulipowafundisheni juu ya ukuu wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo,
hatukutegemea hadithi tupu zisizo na msingi. Sisi tuliuona utukufu wake kwa
macho yetu wenyewe.
17 Sisi
tulikuwapo wakati alipopewa heshima na kutukuzwa na Mungu Baba, wakati sauti
ilipomjia kutoka kwake yeye aliye Utukufu Mkuu, ikisema: "Huyu ni Mwanangu
mpenzi, nimependezwa naye."
18 Tena,
sisi wenyewe tulisikia sauti hiyo kutoka mbinguni wakati tulipokuwa pamoja naye
juu ya ule mlima mtakatifu.
19 Tena,
ujumbe wa manabii watuthibitishia jambo hilo; nanyi mwafanya vema kama
mkiuzingatia, maana ni kama taa inayoangaza mahali penye giza mpaka Siku ile
itakapopambazuka na mwanga wa nyota ya asubuhi utakapong`ara mioyoni mwenu.
20 Zaidi
ya hayo, lakini, kumbukeni kwamba hakuna mtu yeyote awezaye kufafanua mwenyewe
unabii ulio katika Maandiko Matakatifu.
21 Maana
hakuna ujumbe wa kinabii unaotokana na matakwa ya binadamu, bali watu walinena
ujumbe wa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.
|